TIMU Yanga SC imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kujipima nguvu kujiandaa na msimu mpya baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya Mlandege SC usiku wa leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na nyota wa kigeni, Mnyarwanda Patrick Sibomana dakika ya 26, Mganda Juma Balinya dakika ya 36, Mnamibia Sadney Urikhob dakika ya 42 na mzalendo Mrisho Ngassa dakika ya 65.
Bao pekee na la kufutia machozi la Mlandege SC leo limefungwa na Hassan Ramadhani dakika ya 88 na Yanga SC itateremka tena dimbani kesho Uwanja wa Taifa kumenyana na Malindi SC Saa 2:00 usiku pia Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera akizungumza na wachezaji wake wakati wa mapumziko.
*********************************
Mchezo uliopita Yanga SC ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Kariobangi Sharks ya Kenya katika kilele Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuhitimisha.
Awali ya hapo ikiwa kwenye kambi yake ya Morogoro, Yanga SC ilishinda 2-0 dhidi ya Friends Rangers jana, 7-0 dhidi ya ATN, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 1-0 dhidi ya Mawenzi Market.
Na yote hayo ni maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC wakianza na Township Rollers Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, kabla ya kurudiana nao mjini Gaborone kati ya Agosti 24.
Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza Yanga itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Farouk Shikhalo/Metacha Mnata dk46, Paul Godfery/Cleophas Sospeter dk46, Muharami Issa ‘Marcelo’/Jaffar Mohamed dk46, Ally Mtoni ‘Sonso’/Ally Ally dk46, Lamine Moro/Moustafa Suleiman dk46, Papy Tshishimbi/Abdulaziz Makame dk46, Mapinduzi Balama/Mrisho Ngassa dk46, Mohammed Issa ‘Banka’/Feisal Salum dk46, Sadney Urikhob/Maybin Kalengo dk46, Juma Balinya/Issa Bigirimana dk46 na Patrick Sibomana/Deus Kaseke dk46.
No comments:
Post a Comment