*Ilikuwa na kituo kimoja cha kutibu TB mwaka 2015 hadi vituo
103 mwaka 2019.
*Ni miongoni mwa nchi chache duniani yenye kiwango cha chini
cha usugu wa dawa za TB yaani asilimia.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia
Suluhu Hassan, akifungua Mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na
Ukimwi kwa Nchi Wanachama
wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Unaojadili Masuala mbalimbali ya afya, Mikakati dhidi ya
Ukimwi, kuangalia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya
SADC ya Mwaka 1999, Mpango Mkakati wa
Kanda wa Masuala ya Afya na kuridhia kwa pamoja Maazimio mbalimbali
yanayohusiana na Afya kwa Nchi za SADC. Mkutano huo Umefunguliwa leo Novemba 07,2019
katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT CC) Jijini Dar es
salaam.
SERIKALI ya Tanzania imepiga hatua katika kutokomeza ugonjwa
wa kifua kikuu (TB), kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza wakati wa kikao cha mawaziri wa afya na HIV/AIDS
kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Makamu wa
Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam jana, alisema
Tanzania ni miongoni mwa nchi saba duniani zilizofanikiwa kufikia malengo
mkakati ya kutokomeza TB ifikapo mwaka 2020.
Katika kudhihirisha hilo, alisema mwaka 2015 wakati Serikali
ya Awmau ya Tano ikiingia madarakani kulikuwa na kituo kimoja tu kinachotoa
huduma za matibabu ya TB sugu, ambapo hadi kufikia Septemba 2019 vituo 103
vinatoa huduma hiyo.
“Katika mwaka 2018, maambukizi mapya ya TB yamepungua kwa
kasi ya asilimia 4.6 kwa mwaka. Vifo vinavyotokana na TB vimepungua kutoka vifo
55,000 mwaka 2015 hadi vifo 39,000 mwaka 2018 ambayo ni sawa na asilimia 27.
“Utoaji taarifa za wenye TB umeongezeka kwa asilimia 20.6
kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2018. Hii inatokana na kuongezeka kiwango cha
utambuzi wa ugonjwa huu kutoka asilimia 37 mwaka 2015 hadi asilimia 53 mwaka
2018,” alisema Suluhu.
Aidha, alibainisha Tanzania ni miongoni mwa nchi chache
zenye kiwango cha chini cha usugu wa dawa za TB kwa kuwa na asilimia 0.3 ya
usugu kwa wenye maambukizi mapya na asilimia 13 kwa wagonjwa waliokwishatibiwa.
Akizungumzia mikakati ya Serikali ya Tanzania katika sekta
ya afya, Makamu wa Rais alisema: “Kwenye suala la kufikia lengo la afya kwa
wote, Serikali ya tanznaia imeweka kipaumbele katika kuimarisha miundombinu na
mifumo ya afya hususan katika kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa kwa
kuzingaytia ubora na uwiano wa kijiografia.
“Katika kipindi cha miaka mine kuanzia mwaka 2016 hadi 2019
tumefanikiwa kuongeza ujenzi wa vituo vipya vya afya 352 katika maeneo
mbalimbali, ngazi ya kata, hospitali 67 katika ngazi ya wilaya na hospitali
sita za mikoa kwa ajili ya kurahisisha utoaji huduma za afya.”
Alibainisha, serikali imeongeza bajeti katika sekta ya afya
kutika vyanzo vya ndani kuika Sh Bil 30 kwa mwaka 2015/16 hadi kufikia Bil 260
kwama mwaka 2019/20. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Aidha, aliwataka mawaziri wa afya kutoka nchi wanachama za
SADC kujadiliana kwa umakini kwa kuwa matokeo yoyote yanasubiriwa katika nchi
zao kwa manufaa mapana ya jumuiya.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema SADC ilisaini
itifaki ya afya mwaka 1999 ambayo iliridhiwa mwaka 2004 kwa ajili ya kutoa
mwongozo wa masuala ya afya na UKIMWI kwa nchi wanachama.
Ambapo, jumuiya ilianda mpango mkakati wa maendeleo wa kanda
kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.
“Kufuatia hatua hiyo, waheshimiwa mawaziri wamekuwa
wakikutana kila mwaka kama tutakavyokutana leo (jana), kwa ajili ya kupitia
utekelezaji wa program mbalimbali za afya na UKIMWI zilizoainishwa katika
kipengele D cha mkakati huo,” alisema Ummy na kuongeza:
“Kama ilivyo utaratibu wa mikutano hii, wataalamu wa kisekta
walikutana kwa siku tatu kuanzia Novemba 4 hadi 6 kwa ajili ya kujadili na
kutoa mapendekezo juu ya masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya afya na
UKIMWI.”
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji w Sekretariet ya SADC, Dk. Stergomena Tax
alisema kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakikisha nchi wanachama wa SADC wanaimarisha
afya za wananchi kwa kuishi vizuri.
“Tunahitaji mataifa yetu kuendelea kiuchumi, lakini hakuna
uchumi imara bila afya bora. Tumebaini ugonjwa wa Malaria, TB na UKIMWI ni
hatari kwa maendeleo yetu hivyo tumeahidi kupambana nayo hadi kuyatokomeza.
“Hata hivyo, changamoto kubwa tuliyonayo ni rasilimali. Ni
muhimu kuungana pamoja kwa mikakati thabiti ili kutokomeza maradhi na
changamoto za sekta ya afya. Ndiyo maana kesho (leo) tutazindua kampeni ya
‘Zero Malaria starts with me’ maana yake kutokomeza malaria kunaanza na mimi. Hii ni siku ya SADC ya Malaria,”
alisema Dk. Tax.
Tangu Agosti 17, 2019 Tanzania ilipokabidhiwa uenyekiti wa
SADC ambapo kwa sasa Rais Dk. John Magufuli
atashikilia kiti hicho kwa muda wa mwaka mmoja, kumekuwa kukifanyika
vikao vya mara kwa mara vya kisekta ili kufikia malengo ya jumuiya hiyo yenye
lengo la kumaliza changamoto za ukanda huu wa Afrika.
SADC ina wanachama 16 ikiwemo Tanzania, Afrika Kusini,
Botswana, Msumbiji, Angola, Malawi, Zambia, Lesotho, Comoro, Ushelisheli, Mauritius,
Madagascar, Eswatini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe na
Namibia.
Sehemu ya washiriki
Katibu Mkuu wa SADC Dk. Stargomena Tax, akizungumza.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Barnaba Boy, akitoa burudani mbele ya wageni waalikwa katika Mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa sekta ya Afya na UKIMWI (HIV/AIDS) kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika katika Ukumbi wa BOT jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia
Suluhu Hassan, akiagana na Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stergomena Tax
baada ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na Ukimwi kwa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akiagana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Picha ya pamoja...
No comments:
Post a Comment