Habari za Punde

WLAC WALIVYOSHEREHESHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

Mgeni rasmi Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stellah Msophe, akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa mashindano ya kuchora, mwanafunzi wa Shule ya msingi Mburahati, Ibahim Mohamed, wakati wa Tamasha la Siku ya Mtoto wa Afrika lililofanyika katika Viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki .
Mratibu wa Tamasha hilo, kutoka WLAC Abia Richard, akizungumza na kutoa muongozo wa shughuli hiyo.
Mgeni rasmi Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stellah Msophe, akizungumza wakati wa Tamasha hilo.
******************************************
SERIKALI imeweka msisitizo kwa jamii kuendelea kumtambua  mtoto na umuhimu wa mtoto kulindwa ili kuzuia vitendo vya ukatili dhidi yao.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msophe, wakati akihutubia katika Tamasha la Mtoto wa Afrika lililofanyika kwenye Viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. 
Aidha alisema kuwa mtoto ana haki ya kulindwa na mtu yoyote ambapo kwa kufanya hivyo kutaweza kuleta kizazi chenye upendo na endelevu.
Akizungumza katika tamasha la  Siku ya Mtoto wa Afrika lililoandaliwa na Taasisi ya WLAC,  Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msophe amesema serikali imefanya jitihada mbalimbali za kumlinda mtoto ikiwemo kutunga sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Na kuongeza kuwa sheria hiyo imetokana na sera ya mtoto ya mwaka 2008 na kwamba lengo ni kuhakikisha mtoto anatambuliwa, kulindwa na kupatiwa haki zake za msingi.   ''Jamii inapaswa kuhakikisha inamlinda mtoto na kumpatia haki zake ikiwemo elimu, afya na malazi, Ukatili unaofanywa kwa watoto asilimia kubwa hutokana na familia hivyo, tuwalinde watoto wetu. Mtoto hapaswi kubaguliwa," alisema Msophe.
Naye, Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Kinondoni, Agnes Musa alisema kuwa,  wamekuwa wakipokea kesi nyingi za  kulawiti lakini baadhi ya wazazi wamekuwa wakipewa rushwa na wahalifu na kuamua kupuuzia kufuatilia kesi zao. 
Aidha alisema kuwa mashauri yamekuwa yakipelekwa polisi na mahakamani lakini baadae mzazi na muhalifu wanatafutana na kuingia makubaliano ya kupeana fedha, ili umaliza kesi.
 "Wazazi kuahidiwa kupewa Shilingi laki tatu au mbili na inawezekana mtoto kama mwanafunzi anahamishwa shule ili kufuta ushahidi. 
Hata maofisini mwetu kunaletewa mashauri na wakati tunaendelea kuwasikiliza mzazi mmoja anajitokeza na kusema wamefikia makubaliano hii ni changamoto kubwa," 
Alisema kwenye ofisi za ustawi kuna mashauri mengi ya ukatili wa kingono, watoto  kutekelezwa na wengine kukataliwa na kwamba jitihada zao zimewasaidia kuwafanya watoto wengi kusaidiwa.
Alisema ni jukumu kwa wazazi kuwalinda watoto wao kwani kupokea fedha kutoka kwa wahalifu bado hakuondoi mtoto kudhalilika.
Aliiomba jamii isaidie kuibua uovu unaofanywa kwa watoto kwa kuripoti matukio hayo ustawi wa jamii.
" Watoto wajilinde wenyewe, wasipokee zawadi wala kupenda kuomba au kupewa lifti kutoka kwa watu ambao hawawafahamu," alisema
Kwa upande wake, Ofisa wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Kanda Maalum ya Dar es 
Salaam, Leah Mbunda alisema wanaendelea kuelimisha jamii kuhusu ukatili kwa watoto na asilimia kubwa wazazi ndio wanaochangia.
Alisema ulinzi wa watoto unaanzia nyumbani na kwamba watoto wengi wanafanyiwa ukatili kutokana na ukaribu wa ndugu wanaowaona na kuwaamini. Alisema kutengana kwa wazazi kumekuwa changamoto kwa watoto kusababishiwa vitendo vya ukatili.
" Hakuna ushirikiano kati ya wazazi hawafiki kutoa ushahidi mahakamani na sababu ni kukubaliana kinyumbani ili kuepuka adhabu. 
''Wazazi mkumbuke athari zinazowapata sasa hazitafutika hadi ukubwani kwani machangudoa na wezi huanzia hapo," alisema Mbunda.
Mwanafunzi wa Shule ya msingi Kawe A, Adelina Anatory, akipita mbele ya jukwaa kuu kwa mikogo wakati akionesha mavazi.
Wanafunzi wa Shule ya msingi Mzimuni wakiimba shahiri mbele ya jukwaa kuu
Wanafunzi wa Shule ya msingi Anex Mbagala, kutoka (kushoto) Neema Deogratius, Frank Samuel na Laura Charles, wakicheza igizo wakati wa Tamasha hilo.
Igizo likiendelea...........
Wanafunzi wa Shule ya msingi Kawe wakicheza ngoma na mwalimu wao
Wanafunzi wa Shule ya msingi Temeke, wakionesha umahiri wao wa kucheza muziki wa Bongo Fleva.
Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto WLAC, Wakili Theodosia Muhulo, akizungumza wakati wa Tamasha hilo.
Wanafunzi wa Shule ya msingi Mzimuni wakicheza ngoma ya asili. 
Wanafunzi wa Shule ya msingi Kawe, wakicheza ngoma ya asili.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stellah Msophe, akimkabidhi zawadi ya cheti mshindi wa kwanza wa kuchora kwa upande wa Wanawake na wa pili kiujumla Lulu Christopher kutoka Shule ya msingi, Anex.
Mratibu wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Kaanda maalumu, Leah Mbunda, akizungumza.
Mwalimu wa Shule ya msingi, Mburahati, Ester Romani, akiwa katika picha ya pamoja na mwanafunzi wake, Ibrahim Mohamed, baada ya kupokea zawadi ya cheti kuwa msindi wa kwanza katika shule kumi, wa mashindano ya kuchora yaliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto WLAC .
Mratibu wa Tamasha hilo, Abia Richard, akionesha baadhi ya michoro iliyotumika kuwashindanisha watoto.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.