Habari za Punde

UFARANSA YAIKOPESHA TANZANIA SH. BILIONI 195 JUNENGA MRADI WA MAJI SHINYANGA

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia), Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaoui (katikati) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen (kushoto), wakisaini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa shilingi bilioni 195 uliotolewa na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Shinyanga (SHUWASA), Jijini Dar es Salaam.Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia), Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaoui (katikati) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen (kushoto), wakibadilishana mikataba ya mkopo wenye masharti nafuu wa shilingi bilioni 195 uliotolewa na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Shinyanga (SHUWASA), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia), Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaoui (katikati) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen (kushoto), wakionesha wanahabari na wadau walioshuhudia utiwaji Saini mikataba ya mkopo wenye masharti nafuu wa shilingi bilioni 195 uliotolewa na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Shinyanga (SHUWASA),Meza Kuu kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaoui, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhe. Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya hafla ya utiaji Saini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa shilingi bilioni 195 uliotolewa na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Shinyanga (SHUWASA), Meza Kuu kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaoui, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhe. Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba, wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa AFD baada ya hafla ya utiaji Saini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa shilingi bilioni 195 uliotolewa na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Shinyanga (SHUWASA)

******************************************

Na Eva Ngowi, Dar es Salaam
Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la Ufaransa (AFD), imetia saini mkataba wa kuipatia Tanzania mkopo wa Euro milioni 75 sawa na takriban shilingi bilioni 195 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Mkoa wa Shinyanga. 
Akiongea baada ya kusaini mkataba huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel M. Tutuba, alisema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kutoa huduma za uhakika na endelevu za upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Shinyanga.
Bw. Tutuba alisema kuwa mradi huo utaboresha afya, ustawi wa jamii na hali za maisha ya wanufaika wa mradi huo kwa kuboresha na kuimarisha miundombinu iliyopo na kuongeza ufanisi wa uendeshaji na utoaji wa huduma bora kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA). 
“Hii ni ajenda kubwa  inayoendana na hatua za Serikali, kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaotoa vipaumbele pamoja kuboresha upatikanaji na usamabazaji wa Maji na huduma za usafi wa mazingira mijini na vijijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira na ufadhili huu wa AFD utachagia kufikia moja ya vigezo vya Mpango huo wa kuongeza asilimia ya watu wa mijini wanaopata huduma ya maji safi”. Alisema Bw. Tutuba
Bw. Tutuba aliongeza kuwa Mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia 95 katika Manispaa ya Shinyanga na baadhi ya miji midogo katika Wilaya ya Shinyanga, na itawanufaisha wananchi zaidi ya 306,566. 
“Uzalishaji wa maji utaongezeka  kutoka mita za ujazo za sasa ambazo ni 25,877 kwa siku, hadi 33,944; na kuongeza nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika maeneo yanayozunguka mradi” alisisitiza Bw. Tutuba 
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Tutuba alizitaka taasisi zitakazotekeleza mradi huo (Wizara ya Maji na SHUWASA) chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Sanga, watumie uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Sekta ya Maji Tanzania, Programu ya huduma endelevu za Maji na usafi wa Mazingira vijijini na  miradi mbalimbali ya maji na usafi wa mazingira iliyofadhiliwa na AFD ili kutoa huduma nzuri kwa ajili ya wananchi wa Shinyanga na nchini kwa ujumla.
Aliihakikishia Serikali ya Ufaransa kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan iko tayari kuendelea kuimarisha uhusiano wa kimaendeleo kwa faida ya wananchi wan chi hizo mbili na itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati. 
Kwa upande wa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaoui alisema kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika sekta hiyo ambapo katika kipindi cha miezi mitano tu iliyopita kuanzia mwezi Februali, Ufaransa imeipatia Tanzania Euro milioni 330 kiasi ambacho ni kikubwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini.
“Nchi zetu mbili zina urafiki ambao umekuwa ukikuwa kama inavyojidhihirisha katika miradi ya kimaendeleo tunayofadhili ikihusisha mkataba tuliosaini leo.  Tutaendelea kushirikiana hasa katika sekta hizi tatu ambazo ni Maji na Usafi wa Mazingira, Nishati na Usafirishaji na Uchukuzi.” Alisema Mhe. Hajlaoui
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) nchini Tanzania Bi. Stephanie Mouen, alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni moja ya malengo ya kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa. 
Alisema kuwa tangu mwaka 2014 Serikali ya Ufaransa imewekeza zaidi ya euro bilioni 1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo duniani kote ikiwa ni jitihada ya nchi hiyo kuziwezesha nchi zinazoendelea kuondokana na uhaba wa maji na uharibu wa mazingira.
Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, alisema anashukuru kushuhudia kusainiwa kwa mkataba huu wa maji  na usafi wa mazingira kwani utakwenda kusaidia wananchi wa Shinyanga ambao hivi sasa wanapata maji kwa wastani wa asilimia 60. 
Hivyo kukamilika kwa mradi huu kutawezesha maji kufikia asilimia 95 au Zaidi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imeelekeza kufikia mwaka 2025 huduma ya maji mijini ifikie asilimia 95 na maji vijijini ifikie asilimia 85.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa nchi yetu ya kuweza kuaminiwa na nchi mbalimbali, marafiki ambao sasa wanatukopeha kwa masharti nafuu ili kuweza kutekeleza miradi hii ya kimkakati na kuhakikisha kwamba tatizo la maji katika maeneo mbalimbali linamalizika.” Alisema Mhandisi Sanga
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, alisema msaada huu ambao wamekuwa wakitupatia Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Maji pamoja na AFD uendelee kuwepo mpaka mwisho wa kukamilika kwa mradi huu.
“Sisi SHUWASA tuna furaha sana kupokea fedha hizi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu wa Maji safi na usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Shunyanga lakini pia miji midogo ya Tinde, Didia na Isalamagazi maalumu kwa ajili ya kuendeleza huduma za maji safi na Usafi wa Mazingira.” Alisema Mhandisi Katopola

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.