BAADA ya mvutano wa muda mrefu kati ya klabu ya soka ya Geita Gold na mshambuliaji wake mahiri mpachika mabao ambaye aliibuka kidedea na kuwa mfungaji bora msimu uliopita, George Mpole, hatimaye pande zote mbili zimefikia makubaliano ya kusitisha mkataba.
Ofisa Habari wa Geita Gold, Hemed Kivuyo, amesema kuwa pande zote mbili zilifanya mazungumzo ya kina na kukubaliana kuvunja mkataba baada ya kufikia muafaka ili kila mmoja aendelee na maisha yake.
Aidha Kivuyo amesema, awali Mpole alikuwa akiuomba uongozi kusitisha mkataba wake na alikuwa pia akishinikiza kwa muda mrefu kuhusu kuomba kusitisha mkataba wake huo hivyo klabu imeona iachane naye.
“Mpole kwa sasa ni mchezaji huru anayeweza kujiunga na klabu yoyote, Geita Gold inamtakia mafanikio mema katika kuendeleza kipaji chake na soka kwa ujumla,” amesema Kivuyo
Mvutano wa Mpole na Geita Gold ulianza Oktoba 13, mwaka huu baada ya mchezo wa raundi ya saba dhidi ya Coastal Union, ambapo mchezaji huyo aliondoka kikosini kabla ya kurejea siku chache zilizopita.
Novemba 17, mwaka huu uongozi wa Geita ulimpa muda wa wiki moja kurejea kikosini ili kuendelea na programu za timu na kama angekiuka hatua kali za kinidhamu zingechukuliwa dhidi yake.
Na Desemba 4, mwaka huu, Mpole alikuwa sehemu ya kikosi kilichocheza dhidi ya Mtibwa Sugar na kulazimishwa sare ya mabao 2-2, katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, mchezaji huyo akiwa benchi.
Msimu uliopita Mpole aliitwaa kiatu cha dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na jumla ya mabao 17 akiwa mbele ya mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele aliyekuwa na mabao 16.
No comments:
Post a Comment