Habari za Punde

WAZIRI WA FEDHA AKIWASILISHA MAKADIRIO NA MAPATO YA WIZARA YA FEDHA 2024/25

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha, kiasi cha shilingi trilioni 44.19, kati ya makadirio ya shilingi trilioni 49.35 za Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, ili iweze kutekeleza vipaumbele vyake vitano ilivyopanga kuvitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
**********************************
Na Benny Mwaipaja, WF-Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuiidhinishia Wizara yake mapato na matumizi ya jumla ya shilingi trilioni 18.17 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mafungu yake nane (8) ya kibajeti.
Dkt. Nchemba alitoa maombi hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Fedha Jijini Dodoma, ili iweze kutekeleza vipaumbele vyake vitano ilivyopanga kuvitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.63 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha huduma ya deni la Serikali shilingi trilioni 13.13, mishahara shilingi bilioni 946.45, matumizi mengineyo shilingi bilioni 937.30, Huduma za Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi trilioni 2.61 na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 544.05
Dkt. Nchemba, aliliomba pia Bunge kuidhinisha bajeti ya Fungu 045 linalohusisha Ofisi ya Taifa, jumla ya shilingi bilioni 112.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo ambapo kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 101.26 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 11.47 matumizi ya maendeleo. 
Aidha, Dkt. Nchemba alieleza kuwa Wizara yake itatekeleza vipaumbele vitano ikiwemo kutafuta na kukusanya rasilimali fecha kwa ajili ya utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali ambapo imepanga kutafuta na kukusanya shilingi trilioni 44.19, kati ya maoteo ya shilingi trilioni 49.35 za Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho cha shilingi trilioni 44.19 kinachotarajiwa kukusanywa, Mamlaka ya Mapato Tanzania inatarajiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 29.42, misaada na mikopo nafuu shilingi trilioni 5.13, mikopo ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje shilingi trilioni 9.60 na maduhuli shilingi bilioni 45.01. 
“Aidha, Fungu 045 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inakadiria kukusanya shilingi milioni 850 ikiwa ni mapato ya kodi ya pango kutokana na upangishaji wa majengo ya Ofisi yaliyopo katika mikoa mbalimbali nchini” aliongeza Dkt. Nchemba.
Alivitaja vipaumbele vingine vya Wizara kuwa ni kuimarisha na kusimamia mifumo ya mapato, matumizi na mali za Serikali ikiwemo IDRAS, TANCIS, MUSE, NeST, CBMS na GAMIS; Kuhudumia deni la Serikali kwa wakati na kuboresha kanzidata ya kutunza taarifa za deni” alisema Dkt. Nchemba.
“Wizara imepanga pia kutoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za fedha nchini; na Kujenga uwezo kwa wakaguzi wa ndani, kamati za ukaguzi pamoja na waratibu wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma.
Mafungu 8 ya Wizara ya Fedha ni pamoja na Fungu 01- Deni la Serikali, Fungu 06- Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Fungu 10- Tume ya Pamoja ya Fedha, Fungu 13- Kitengo cha Kudhibiti Fedha haramu, Fungu 21- Hazina, Fungu 22- Huduma za Mfuko Mkuu, Fungu 23- Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na Fungu 50- Wizara ya Fedha, huku Fungu 045 – linalosimamiwa na Wizara ya Fedga linalohusisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.