Habari za Punde

*MSONDO WAJUFUA KUWAPAGAWISHA WAGOSI


BENDI Kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Music bendi inatarajia kufanya ziara ya utambulisho wa albam yao mpya ya ‘Huna Shukurani’ ndani ya Mkoa wa Tanga mapema mwezi huu.
Akizungumza na Sufianimafoto jijini Dar es Salaam, Msemaji wa bendi hiyo Rajabu Mhamila 'Super D' alisema sambamba na kutambulisha albamu hiyo pia ziara hiyo ni maalum kwa mashabiki wao wa mkoa huo ikiwa ni onyesho la kwanza kwao tangu kuanza kwa mwaka mpya.
Aidha alisema kuwa onyesho hilo liwakutanisha wapendanao ikiwa ni maadhimisho ya sikukuuu hiyo inayosherehekewa Februari 14, Duniani kote.
“Katika maonyesho hayo yote mashabiki wa Msondo watapata fursa ya kuzikiliza nyimbo mpya za ambazo zimeshaandaliwa maalum kwa ajili ya albam mpya ijayo, pamoja na zile zilizomo kwenye albam ya Huna Shukurani, na nyimbo zote kali zilizotamba katika miaka ya nyuma.”
Alizitaja baadhi ya nyimbo mpya kuwa ni ‘Lipi jema’, uliotungwa na Eddo Sanga, na ‘Dawa ya Deni Kulipa’ uliotungwa na Isihaka Katima (Dj Papa Upanga) ambao tayari umeshakamilika.
Nyimbo nyingine zilizomo katika alabamu hiyo ya Huna Shukrani, ni Kiapo, iliyotungwa na Husein Jumbe, Haki yangu ipo wapi, uliotungwa na Uluka Uvuluge, Mama Cos, uliotungwa na marehemu, Joseph Maina, Albino uliotungwa na Juma Katundu, Machimbo uliotungwanao, Isihaka Katima na Dj Papa Upanga, na Cheo ni Dhamana uliotungwa na Eddo Sanga.
Bendi hiyo itasafiri na wanamuziki wake wote waliotajwa kuwa ni, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Muhidin Gurumo, Rapa wa bendi hiyo Romani Mng'ande 'Romario', na kiongozi wa bendi hiyo Saidi Mabela pamoja na wanenguaji wake, Amina Said 'Queen Emmy' Nacho Mpendu 'mama Nzawisa' na Amiri Saidi 'Dongo'.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.