Habari za Punde

*MAN UTD YAITOA NISHAI MAN CITY, CHELSEA YASIMAMISHWA

Na Sufianimafoto
PAUL Scholes jana alimuonyesha kocha Alex Ferguson kwamba hajakosea kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja zaidi kuendelea kuichezea Manchester United ya England, baada ya kuipatia bao pekee la ushindi wa 1-0 na kuibuka shujaa kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya wapinzani wao, Man City, Uwanja wa Eastlands mjini Manchester.
Kiungo huyo mkongwe, aliifungia timu yake bao katika dakika za majeruhi, baada ya kuunganisha krosi ya Patrice Evra hivyo kuifanya Man United kufikisha pointi 76 katika mechi 35 ilizocheza.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha shangwe na vifijo kwa mashabiki wa Man United ambao waliamini timu yao ingeambulia sare ya 0-0 lakini Scholes alifanya maajabu mara baada ya mwamuzi wa akiba kuonyesha ubao wa dakika 3 za nyongeza na ndipo alipofunga bao katika dakika ya pili.
Katika mechi ya jana timu zote zilicheza kwa kukamiana na kushambuliana mara kwa mara ambako Evra alilimwa kadi ya njano kwa upande wa Man United wakati Kompany na Johnson nao walipewa kadi kama hiyo kwa upande wa Man City.
Matokeo hayo ni wazi yanakuwa mabaya zaidi kwa City ambao harakati zao za kusaka nafasi nne za juu katika ligi hiyo ni kama zimeingia doa kwani wanabaki na pointi zao 62 katika mechi 34.
Katika kuimarisha kikosi chake, Kocha wa Man City, Roberto Mancini aliwatoa, Kompany na kumuingiza Patrick Vieira, Do Jong na kumuingia Stephen Ireland na Emmanuel Adebayor ambaye nafasi yake ilichukuliwa Shaun Wright Phillips.
Kwa upande wa Man United, Sir Alex Ferguson aliwatoa Valencia na kumuingiza Obertan, Gibson alimpisha Nani na Rooney nafasi yake ilichukuliwa na Berbatov.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika mechi ya Kombe la Ligi, Januari mwaka huu, Man United ilishinda kwa mabao 3-1 huku wafungaji wakiwa ni Scholes, Carrick na Rooney wakati bao pekee la City lilifungwa na Tevez.
Wakati huo huo Chelsea pia jana ilisimamishwa kwa kupigwa na Tottenham mabao 2-1, na hivyo kifanya kubaki na point 77 akiwa mbele kwa point moja dhidi ya Man U, huku kila mmoja akiwa amebakiza mechi tatu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.