*ABDULHALIM HUMUD ACHEMSHA ACHEZA DAKIKA CHACHE NA KUTOLEWA
Timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, inayoshiriki katika mashindano ya Kombe la kagame yanayoendelea huko nchini Rwanda, leo imeshindwa kuonyesha cheche zake mbele ya kimnyama kidogo, 'Paka', yaani Sofapaka ambao ni mabingwa wa soka wa nchini Kenya baada ya kufungwa bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, Simba, iliyoshinda mchezo wake wa kwanza dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe hilo, timu ya Atraco ya Rwanda mabao 2-1, inahitaji ushindi katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya mabingwa wa Uganda, timu ya URA, ili iweze kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa vilabu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Sofapaka, ambayo iliwahi kuifunga Simba katika michuano ya Kombe la Tusker iliifunga, ilicheza kwa juhudi na kuweza kupata ushindi huo.
Sofapaka imetinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya Kagame ikiwa ni timu ya kwanza kutoka katika kundi C.
Pambano hilo lilianza kwa Simba kulishambulia lango la Sofapaka, Dakika 15 za kipindi cha kwanza Simba ilicheza mchezo maridadi wa kusisimua, na katika dakika ya 11 mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka African Lyon, Robert Sentongo, alifunga bao, lakini mwamuzi wa mchezo huo, Mohamed Ally Farah kutoka Djibout alikataa bao hilo kwa madai kuwa mfungaji alikuwa ameotea.
Simba iliendelea na mashambulizi ambapo dakika ya 24, Mussa Hassan Mgosi alipata nafasi nzuri ya kufunga, lakini hakuweza kuitumia vyema, na kadi kumalizika kwa mchezo huo Simba haikuweza tena kuonyesha cheche zake na kuruhusu mashambulizi langoni mwao.
Sofapaka ilipata bao dakika ya 30 lililofungwa na John Barasa.
Katika kipindi hicho cha kwanza Simba ilikuwa ikiruhusu mashambulizi na kama si uimara wa kipa wao, Juma Kasseja, Sofapaka ingeweza kupata mabao mengi zaidi.
Mchezaji mpya wa Simba liyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, Abdulhalim Humud, akiichezea Simba kwa mara ya kwanza alishindwa kumudu mchezo huo na kutolewa baada tu ya dakika tano (5) kabla ya mapumziko, nafasi yake ikachukuliwa na Nico Nyagawa.
No comments:
Post a Comment