Habari za Punde

*YANGA YAMTEMA RASMI MANJI





Na Sufianimafoto Reporter, jijini

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeamua kumpunguzia mzigo mfadhili wao mkuu, Yusuph Manji, kwa kumlipa kocha wao Mkuu Mserbia, Costadin Papic, badala ya kocha huyo kulipwa na Manji.

Akizungumza leo Dar es Salaam, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema kuwa uamuzi huo umetolewa na kamati ya utendaji ya klabu iliyokutana hivi karibuni.

“Viongozi wameamua katika mkataba mpya ambao Papic atasaini, klabu itakuwa ikilipa tofauti na awali ambako alikuwa akilipwa na Manji,” alisema Sendeu.

“Uongozi umeamua kuwa klabu ndiyo itakuwa ikimlipa kocha na si Manji tena, hii imeonekana kuwa ana mzigo mkubwa, hivyo jukumu hilo tumeamua kuwa klabu ndiyo ibebe,” alisema Sendeu.

“Mfadhili wetu amekuwa akitufadhii vitu vingi, ikiwamo kulipa wachezaji mishahara, tunapokwenda kuweka kambi maalumu amekuwa akitupa fedha za kulipia kambi hiyo, hivyo tukaona tumsaidie kumlipa kocha,” alisema Sendeu.

Sendeu alisema kuwa kwa kuamua kumlipa kocha huyo, klabu hivi sasa imeonyesha kupiga hatua, ikiwa ni pamoja na kuonyesha kuwa ina uwezo wa kujitegemea na si kuwa tegemezi kwa kila kitu kwa mfadhili.

Sendeu alisema kuwa hivi sasa klabu inaendelea na mazungumzo na kocha huyo.

Mbali na Yanga kufanya mazungumzo na kocha huyo, habari kutoka TFF zinasema kuwa kocha huyo ndiye atakayemrithi kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars) Marcio Maximo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.