MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete,ameahidi kujenga upya bandari ya Mbamba Bay pamoja na kununua Meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400.
Alitoa ahadi hiyo jana wakati akinadi sera kwenye kampeni katika jimbo la Mbinga ambapo alisema bandari hiyo itaendana na hadhi ya wilaya mpya ya Nyasa itakayoanza kutumika mwakani.
Aidha, Kikwete pia aliahidi kutengeneza utaratibu mzuri wa biashara kati ya Malawi na Tanzani ili nchi hizo mbili ziweze kuuziana bidhaa.
"Mimi nasema nitanunua meli, wenzangu wanachukia, sasa hawataki wenzao wapate usafiri.
Wao wanaahidi treni ya kutoka Dar es Salaam kwenda
Mwanza kwa saa tatu na vitu vingi bure, hatusemi, wanahofia ahadi zetu ni za kweli zao za uongo." alisema Kikwete.
Katika sekta ya kilimo alisema ahadi kubwa ni kutekeleza sera yakilimo kwanza ambayo ni kuongeza kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, mbolea, kuongeza idadi ya mabwana na bibi shamba na kupunguza matumizi ya jembe la mkono katika miaka mitano ijayo.
Awali akimkaribisha mgombea urais, mgombea ubunge wa jimbo hilo Kapteni John Komba alisema, jimbo hilo linakabiliwa na kero za ulanguzi wa sukari, bandari na uvuvi.
Alisema sukari iliyopo ni ya magendo kutoka nchi jirani ya Malawi,ambayo huuzwa kwa sh. 1500 kwa kilo moja tofauti na ya Tanzania ambayo huuzwa sh. 3000-3500.
"Tunaiomba serikali itusaidie ituruhusu tufanye biashara na Malawi kihalali, tuwapelekee mpunga na mahindi watuletee sukari pia itusaidie namna gani tutakua na dagaa katika ziwa Nyasa, utafiti ufanyike bila kuathiri mazalia ya samaki." alisema.
Komba alisema mbali na kero hizo pia Nyasa kabla ya kuwa wilaya ilikua nyuma kimaendeleo ambapo kwa sasa imepiga hatua katika sekta ya Afya ambapo ina hospitali mbili mbali na ile moja ya zamani.
Alisema ingawa hospitali hizo ni za mashirika ya dini lakini serikali ina mkono wake katika kuwalipa madaktari pamoja na dawa.


No comments:
Post a Comment