WANANCHI wa Jimbo la Liwale, mkoani Lindi, wameaswa kuvunja makundi na kuunganisha nguvu zao pamoja ili waweze kuijenga upya wilaya yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Liwale kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Faith Mitambo, wakati wa ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge wao.
Bi. Mitambo amesema kazi kubwa ya mbunge ni kushirikiana na wananchi kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana, hivyo akawaasa kuwa iwapo watashirikiana nae vizuri katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake mabadiliko yataonekana.
"Ndugu zangu wana Liwale, kipindi cha misukosuko ya uchaguzi kimeisha, mbunge wa jimbo letu amepatikana, ambaye ni mimi Faith Mitambo, kazi yangu ni kushirikiana nanyi kuleta mabadiliko," amesema Bi. Mitambo.
Amewaambia wananchi kuwa miaka mitano ya uongozi wake, anakabiliwa na changamoto nyingi, ambazo iwapo atapata ushirikiana mzuri kutoka kwa wananchi na watendaji wa halmashauri, kwa pamoja watafanikiwa.Naye Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Bw. Paul Chiwile, alimwambia Bi. Mitambo kuwa baada ya wabunge kuapishwa mjini Dodoma, wananchi walilipuka kwa furaha, jambo ambalo lilionesha kuwa na imani naye.Mkuu huyo wa wilaya alisema alipofika Liwale kama Mkuu wa Wilaya mwaka 2009, hapakuwa na mawasiliano kati yake na mbunge, jambo ambalo ni mzigo katika kuendesha Serikali."Sikuwa na mawasiliano na mbunge aliyepita, hakukuwa na utaratibu wa kuonana wala kubadilishana mawazo, nilifanya kazi kwa wakati mgumu sana, kuchaguliwa kwa Bi. Mitambo na kuapishwa kumenipa faraja sana," alisema.
Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Liwale, Bw. Mohamed Ngomambo, amesema jimbo hilo limepata kiongozi imara katika ngazi ya ubunge na kuwaasa wananchi kumtumia vizuri ili kuharakisha maendeleo.Katika ziara hiyo, Bi. Mitambo alikabidhi msaada wa darubini mbili zenye thamani ya sh. milioni 3 kwa Hospitali ya Wilaya ya Liwale na baiskeli tano za kubeba wagongwa, baiskeli 45 za walemavu wa viungo, kompyuta moja kwa CCM na sh. milioni 1 kwa mtandao wa akinamama wajasiriamali (WAMALI).
No comments:
Post a Comment