Habari za Punde

*GAVANA NDULU AWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU NOTI MPYA


Imeelezwa kuwa hali ya kuacha rangi noti zinaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe ni kwa lengo kwa sababu ya kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kuchanika na kuchakaa haraka.
Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Beno Ndulu alisema noti inaposuguliwa kwa nguvu kwenye karatasi nyeupe ni uthibitisho kuwa noti hiyo ni halali.
Profesa Ndulu alisema hali hiyo ni moja ya usalama inayothibitisha kuwa noti hizo si bandia na siyo bandia.
Aliendelea kusema kuwa noti halali zikilowekwa kwenye maji hazichuji kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi kwa kuwa wino uliotumika hauyeyuki katika maji.
Aliongezea kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ya kuwekewa kinga dhidi ya uchafu inayojulikana kitaalamu kama Anti Soiling Treatement ili kupunguza uwezekano wa kunasa uchafu inapokuwa katika mzunguko.
Amewashauri wananchi kuzichunguza kwa makini noti mpya kwa kutumia alama za usalama za Mwalimu Nyerere inayoonekana inapomulikwa noti kwenye mwanga ikiwa ni pamoja na kuipapasa ili kuhisi mparuzo kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalum.
Alama nyingine ni kukagua utepe maalumu kwenye noti za shilingi 500/=, 2000/=, 5000/= na 1000/= ambao unaonekana kama madirisha yenye umbo la almasi ambao hubadilika badilika noti inapogeuzwa geuzwa.
Alizitaja alama nyingine ni kutumia taa maalumu yenye mwanga wa dhambarau ili kuhakiki alama maalumu zilizooneshwa kwenye vipeperushi na matangazo ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kukuzia maandishi madogo yaliyooneshwa kwenye vipepereshi na matangazo.
Profesa Ndulu alisema mikakati ya Benki kuu ni kufikisha elimu ya “tambua noti zako” kwa wananchi wote kupitia matangazo,Semina,Ushiriki katika mikusanyiko mikubwa kama sabasaba na nanenane pamoja na minada mikubwa ya mifugo.
Hivi karibuni baadhi ya wananchi wamekuwa na hofu juu ya noti mpya kwa madai kuwa zinachuja rangi hali ambayo imezua utata kwa wananchi wengi.
Mtaalamu aliyetengeneza fedha hizo, akitoa mfano wa kuhakiki noti bandia na ile isiyo bandia kwa kuonyesha jinsi ya kuweza kuzigundua kwa kutumia karatasi nyeupe na kuisugua noti hiyo, ambapo kama si feki alidai ni lazima itoe vumbi la rangi ya noti hiyo na kama ni feki basi haitoa vumbi hilo kamwe.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.