Na www.BBC Swahili.com
Mapigano baina ya waasi na majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi yamekuwa yakiendelea katika miji muhimu baada ya mashambulio ya anga yanayoendelea kwa mfululizo wa siku ya tano sasa yanayofanywa na majeshi ya kimataifa.
Milio mingi ya milipuko ilisikika usiku kwenye mji mkuu wa Tripoli.
Katika mji unaoshikiliwa na waasi Misrata, mashariki mwa Tripoli, vifaru vya serikali vimekuwa vikishambulia eneo karibu na hospitali.
Kumekuwa pia na ripoti juu ya mapigano makali baina ya waasi na majeshi yanayomwuunga mkono Gaddafi mjini Ajdabiya.
Wakazi waliokimbia mji huo wameelezea kuwepo kwa makombora, milio ya risasi na nyumba kuwashwa moto.
Mashambulio ya anga
Kulingana na vyanzo vya jeshi vya Libya na vyombo vya habari vimesema, kuna ripoti za kuwepo mashambulio ya anga yaliyofanywa na nchi za magharibi kwenye mji wa Tajura.
Na jeshi la Ufaransa limesema mashambulio ya anga yaliyofanywa na Ufaransa yamelenga kituo cha anga cha Libya ndani ya nchi hiyo nyakati za usiku.
Siku ya Alhamis, ndege za kijeshi za nchi za magharibi zimeripotiwa kushambulia mji wa Sebha kusini mwa Libya, kulingana na wakazi na taarifa kutoka vyombo vya habari.
Sebha, uliopo kilomita 750 kusini mwa Tripoli, ni eneo lililodhibitiwa vilivyo na ni kitovu cha kijeshi cha Kanali Gaddafi.
Pia kumeripotiwa kuwepo kwa mlipuko nyakati za usiku kwenye kituo cha kijeshi eneo la Tajura mashariki mwa Tripoli.
No comments:
Post a Comment