JESHI la Polisi wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga linamshikilia kijana Tano Sita, mkazi wa kijiji cha Mwamala wilayani Nzega mkoa wa Tabora, aliyekamatwa akiuza kichwa cha mkewe pamoja na viungo vingine vya mwili wa mkewe, matiti na sehemu za siri.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Diwani Athuman, alisema Katinda alikamatwa na polisi katika eneo la benki ya CRDB tawi la Kahama akitaka kuwauzia viungo hivyo polisi waliokuwa kwenye lindo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, Katinda alikamatwa jana asubuhi baada ya kufika katika eneo hilo akidai anauza nyama ya nguruwe iliyokuwa kwenye mfuko wa sandalusi hali iliyomfanya kila mtu aliyekuwa katika eneo hilo kubaki na mshangao kwa kile kilichokuwa kikiendelea.
Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kufika eneo hilo askari aliyekuwa kwenye lindo pamoja na wenzake, baada ya kuiangalia nyama hiyo iliyodaiwa kuwa ni ya nguruwe cha ajabu waliona kichwa cha binadamu kikiwa pamoja na viungo hivyo na ndipo walipomweka chini ya ulinzi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi, awali kijana huyo alionekana kwenye eneo la stendi ya mabasi maeneo ya CCM Kahama akiuza viungo hivyo ndipo alipoelekezwa kwenda kuuza kwa maaskari waliokuwa katika lindo la benki za CRDB na NMB, bila watu hao kujua kuwa kijana huyo amebeba nini katika furushi lake.
Aidha alisema kuwa baada ya kufika benki ya NMB, aliwaambia maaskari hao kuwa anauza kitimoto lakini walimjibu kuwa wao ni Waislamu hawatumii nyama hiyo na kumwelekeza kwenda kwa askari waliokuwa wakilinda benki ya CRDB ndipo alipokamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha wilaya.
Alisema kijana huyo baada ya kukamatwa alikiri kuwa viungo hivyo vilikuwa ni vya mkewe aliyemtaja kwa jina la Kabula Luziga (18) mkazi wa Itobo, wilayani Nzega.
Baada ya kijana huyo kuhojiwa, alisema alimuua mkewe usiku kwa kutumia panga baada ya kumvizia akiwa amelala huku kiwiliwili cha mwili wa marehemu Luziga, akikiacha katika chumba chake nyumbani kwa Babu yake aliyemtaja kwa jina moja la Mwanandilila katika kijiji cha Mwamala wilayani Nzega, mkoani Tabora.
Kamanda alisema baada ya kumhoji kijana huyo alidai kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kusikia matangazo kwenye redio moja ya mjini Kahama kuwa viungo hivyo vinahitajiwa na kuna wateja wa kununua ndipo alipoamua kumuua mkewe.
No comments:
Post a Comment