Habari za Punde

*MCT KUTOA TUZO ZA WAANDISHI BORA MEI 3 MWAKA HUU MLIMANI CITY

Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika moja ya kazi zao.

Na Sufianimafoto Reporter, jijini
KAMATI ya Maandalizi ya Tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT), imeandaa usiku maalum ambapo kutakuwa na hafla ya kuwazawadia waandishi wa habari waliofanya vizuri katika makundi mbalimbali ya uandishi kwa mwaka 2010.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, jijini Dar es Salaam, leo mchana, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema kuwa half hiyo itafanyika Mei 3 katika Ukumbi wa Mlimani City Mwenge jijini.
Aidha alisema kuwa Kamati ya Maandalizi ya hafla hiyo, itaongozwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA), Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), HakiElimu na Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET).
Vyama vingine vitakavyoshirikishwa ni pamoja na Taasisi ya Uandishi wa habari Kusini mwa Afrika-Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Chuo cha Johns Hopkins na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT).

Mukajanga aliwataka waandishi wa habari wanaohitaji kushiriki mashindano hayo ya tuzo, kutuma kazi zao zilizoishachapishwa katika magazeti au kutangazwa Redioni na Televisheni kuanzia January 1, 2010 hadi Desemba 31 2010.

Aidha alisema kuwa Fomu za ushiriki zinapatikana MCT, kwenye Tovuti ya MCT na pia zitasambazwa katika Klabu za waandishi wa habari Ofisi za Vyombo vyote.

“Majaji watakuwa wakiangalia iwapo habari inayoshindanishwa kama inasaidia kutoa maarifa mapya kuhusu suala muhimu katika jamii na upekee wa kazi ya mwandishi, ubunifu, utafiti na ubora na ubora wa namna kazi ilivyowasilishwa, umahiri katika kutumia lugha, kiwango cha kufuata maadili ya kitaaluma ikiwa ni pamoja na kusema ukweli, usahihi, ustaarabu na kuweka wazi katika habari.

Katika tuzo za mwaka huu waandishi watatakiwa kushindanisha kazi zao katika makundi 16, yafuatayo:-

1:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Utawala Bora, Upande wa magazeti, redio na televisheni.
2:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Jinsia upande wa magazeti, redio na televisheni.
3:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Uchumi na Biashara, upande wa magazeti,redio na televisheni.
4:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Michezo na Utamaduni, upande wa magazeti redio na televisheni.
5:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Mazingira, upande wa magazeti, redio na televisheni.
6:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Afya, upande wa magazeti, redio na televisheni.
7:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, upande wa magazeti na televisheni.
8:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Malaria,upande wa magazeti, redio na televisheni.
9:-
Tuzo ya Uandishi wa habari za Watoto, upande wa magazeti, redio na televisheni.
10:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Elimu, upande wa magazeti, redio na televisheni.
11:- Tuzo ya Uandishi wa habari kuhusu kazi na Mahusiano kazini, kwa upande wa magazeti, redio na televisheni.
12:- Tuzo ya Mpigapicha Bora.
13:- Tuzo ya Mchoraji Bora wa Vibonzo.
14:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Mawasiliano, upande wa magazeti, redio na televisheni.
15:- Tuzo ya habari za Sayansi na Teknolojia, upande wa magazeti, redio na televisheni.
16:- Tuzo ya Uandishi wa habari za Watu wenye ulemavu, upande wa magazeti, redio na televisheni.

Kajubi alisema kuwa kutakuwapo na kundi la wazi ambalo litakuwa ni kwa ajili ya waandishi wa habari ambao kazi zao hazikuweza kuingia katika makundi yaliyotajwa hapo juu.
Washindi wa kila kundi watazawadiwa vyeti, vikombe na zawadi ambazo zitatangazwa baadaye, pia kutakua na mshindi wa jumla ambaye atafaidika kwa kugharamiwa masomo katika fani yeyote inayohusiana na habari ilimradi gharama yake isizidi Dola za Kimarekani 4,000.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.