SERIKALI imetoa tamko la kusaidia kupatikana kwa wanamuziki wengine watakaounda kundi la taarabu la Five Stars Modern Taarab baada ya wanamuziki 13 wa kundi hilo kupoteza maisha katika ajali iliyotokea hivi karibuni mkoani Morogoro.
Akizungumza katika dua ya kuwaombea wanamuziki hao juzi katika hoteli ya Starlight, Naibu Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Dr Fenela Mukangara alisema vijana wasikate tamaa baada ya vijana hao kupoteza maisha katika ajali hiyo.
Mukangara alisema serikali katika jitihada za kufanikisha azma hiyo watajitahidi kuwasiliana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuzipiga nyimbo za kundi hilo na kusaidia kuuza kazi zilizofanywa na kundi hilo .
Aidha Mukangara alisema Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano kwa muda wote viongozi na familia za marehemu waliokumbwa na msiba huo hapa nchini.
Mukangara alisema watajipanga kuwasaidia vyombo kundi hilo kwa kushirikiana na wadau wa muziki hapa nchini baada ya kundi hilo kupoteza pia vyombo vyake katika ajali hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Henry Clemence alitoa wito kwa wasanii kutunga tungo za kupigia kelele madereva wazembe kwa sababu ajali ndio mojawapo ya matukio yanayomaliza Watanzania wengi.
Clemence ambaye pia ni Mwenyeji wa wanachama wa Taasisi ya Wasanii Tanzania (SHIWATA), Wilayani Mkuranga alisema pengo la wanamuziki hao halitozibika.
Mwenyekiti wa Shiwata, Taalib Cassim alitoa shukrani kwa viongozi wa Serikali kwa kuonyesha kuwajali wasanii ambako Asilimia kubwa ya viongozi wa serikali kupitia Wizara kuhudhuria katika dua ya kuwaombea marehemu walifariki katika ajali hiyo.
Cassim alisema Shiwata inawapenda viongozi wa Serikali kwa kuonyesha kuguswa na tukio hilo ambalo limetingisha Taifa.
Viongozi waliohudhuria katika dua hiyo iliyoandaliwa na Shiwata ni pamoja na Mkurugenzi wa Utamaduni, Profesa Hermas Mwansoko, Msaidizi wake Anjela Ngowi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ghonche Materego na wadau mbalimbali wa sanaa.
No comments:
Post a Comment