*************************************
Na. Hillary Shoo, Singida.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mohammed Dewji (MO) ametoa posho ya Sh. 50, 000 kwa jumla ya walimu 808 wa Manispaa ya Singida mjini na kuwashangaza walimu wa shule za Msingi Manispaa ya Singida wakati wa hafla fupi ya kuzungumzia changamoto zinazowakabili walimu hao.
“Ndugu zangu walimu kwa kuwa leo hii nimefurahi kukutana nanyi hapa na kuzungumzia changamoto zinazowakabili katika kutekeleza kazi zenu za kila siku posho ya leo kila mwalimu atapata shilingi 50,000 .” alisema MO na kusababisha ukumbi mzima kulipuka kwa nderemo na vifijo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki na walimu hao kwenye ukumbi wa chuo kipya cha ualimu Misuna Dewji aliwashukuru walimu kwa kukichagua chama cha CCM na kukipa ridhaa ya kuongoza nchi.
Aidha alisema heshima waliyompa pamoja na wananchi wa jimbo hilo anaienzi na kuithamini kwa moyo wake wote kwani anatambua umuhimu wao katika jimbo hilo “Nani kama mwalimu, walimu waliitikia hakuna.”
Mapema Kaimu Ofisa Elimu wa Manispaa ya Singida Ramadhan Labito alimweleza Mbunge kuwa walimu wanakabiliwa na changamoto nyingi ikwemo ukosefu wa madawati na uchakavu wa vyumba vya madarasa katika shule nyingi za msingi.
Labito alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa nyumba za walimu maeneo ya vijijini, kukopeshwa vyombo vya usafiri, kupatiwa viwanje vyenye hati, kupatiwa mikopo mbalimbali yenye masharti nafuu, kuimarishwa kwa vituo vya kulelea watoto yatima kititimo na Kompyuta mashuleni.
Zingine kwa mujibu wa Kaimu Ofisa elimu Labito ni kuchimbiwa visima vidogo mashuleni ili upatikanaji wa maji kwa ajili ya kutunza mazingira ya shule yawe mazuri, kuuziwa vifaa vya ujenzi kwa bei poa pamoja na umeme wa jua kwa maeneo ya vijijini.
Akijibu changamoto hizo MO alisema amezipokea na zile ambazo ana uwezo nazo atazitekeleza mwenyewe haraka iwezekanavyo lakini nyingine ambazo ziko nje ya uwezo ataziwasilisha serikalini kwa ajili ya utekelezaji.Walimu wakilipuka kwa nderemo na vifijo mara baada ya MO kuwatangazia posho ya 50,000 kila mmoja walimu hao.
No comments:
Post a Comment