Baadhi ya Wananchi wa Kitogoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, wakipita pembezoni mwa uzio wa senyenge iliowekwa na kampuni ya Tanbreed Poultry Limited, inayomilikiwa na Raia wa kigeni aliyeuziwa eneo hilo kubwa la ardhi na kumega sehemu ya mashamba ya wanakijiji wenye mazao ndani ya uzio huo na kuziba njia ya kuwawezesha kupita na kufika katika mtaa wa Mwanga kama walivyokutwa juzi Kijijiji hapo. Picha na Mroki Mroki
Bibi Mawazia Kibwana, mkazi wa Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, akitoa malalamiko kuhusu kubomolewa choo chake na kuwekwa kwa uzio wa senyenge na kampuni ya Tanbreed Poultry Limited inayomilikiwa Raia wa kigeni aliyeuziwa eneo kubwa la ardhi na kumega sehemu ya mashamba yao wenye mazao.
Mkazi wa Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, Ally Kidunda, akizungumza katika mkutano wa hadhara uliokuwa uzikutanisha pande mbili za wakulima wa kijiji hicho na mzungu anayemiliki kampuni ya Tanbreed Poultry Limited inayodai kununua shamba katika kitongoji cha Kinyenze na kumega sehemu ya mashamba yao yenye mazao ndani yake na kuziba njia.
*****************************************
Na Mroki Mroki, Mvomero
*Wananchi waitaka Serikali ya wilaya na mkoa kuingilia kati harakaWANANCHI wa Kitongoji cha Kinyenze , Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali , Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamewataka viongozi Wilaya na Mkoa huo kuingilia kati haraka mgogoro wa ardhi baina yao na mwekezaji wa Kigeni aliyeuziwa shamba kijijini hapo.
Wananchi hao pia wamewashutumu baadhi ya Viongozi wa Serikali ya Kijiji hicho na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya kwa kushindwa kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mipaka ya ardhi kati ya Kijiji na Mwekezaji huyo ambaye ni Raia wa Kigeni mmiliki wa Kampuni ya Tanbreed Poultry Limited aliyeuziwa shamba kijijini hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano wa hadhara uliokuwa na lengo la kuzikutanisha pande mbili zenye mgogoro wa mipaka ya ardhi chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo na maofisa wake wa Idara ya Ardhi ili kutafuta suluhu ya sakata hilo, ambapo wakazi hao wameulaumu Uongozi wa Halmashauri kwa kushindwa kutokea mkutanoni hapo na mwekezaji huyo.
“Kitendo cha Viongozi kupanga tarehe ya mkutano na kushindwa kufika bila sababau za msingi ni dharau kubwa kwetu wananchi na endapo tatizo tulilonalo halitashughulikiwa haraka, sisi tutachukua maamuzi yetu wenyewe ya kubomoa uzio uliowekwa na muwekezaji huyo na lolote litokee”, alisema Shaban Maguo.
Viongozi waliopaswa kufika katika mkutano huo ambao hawakufika ni Pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvovero, Maofisa wa Ardhi, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kipera, na Ofisa Mtendaji wa Kata ambaye alifika eneo hilo la mkutano na kutoweka katika mazingira ya kutatanisha bila kuaga baada ya kukuta waandishi wa habari lukuki wakiwa wamejivinjari eneo hilo la mkutano ili kujua juu ya muafaka wa sakata hilo endapo mkutano huo ungefanyika.
Wananchi hao walishagazwa kuona Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, ambao waliandika barua ya kuutaka Uongozi wa Serikali ya Kijiji kuitishwa mkutano wa pamoja wa pande hizo, Agosti 23, mwaka huu , lakini walishindwa kutokea pamoja na Ofisa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji pamoja na Mwekezaji huyo ambaye ni Mmiliki wa Kampuni ya Tanbreed Poultry Limited inayomilikiwa na Mzungu.
Mkazi wa Kitongoji hicho ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kipera, Ally Kidunda, alidai kuwa kushindwa kutokea kwa viongozi hao ambao waliandaa barua hiyo na kupanga siku ya mkutano huo, kinawatia wasi wasi juu ya kutaka kuficha ukweli wa mambo.
“ Sisi hatuna imani na Viongozi wetu , kama wao ndiyo wameandika barua yenye kumbukumbu namba MVDC /V.10/4/12 ya Agosti 4, mwaka huu na kutaja tarehe 23 mwezi huu ni siku ya kufanyika mkutano wa pamoja wa mgogoro wa shamba namba 296 Kinyezi , Kipera, Wilaya ya Mvomero, lakini wameshindwa kutokea” Kidunda alishangazwa na jambo hilo.
No comments:
Post a Comment