Mtoto Cecilia Edward ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo uliopelekea kuvimba kwa tumbo amewashukuru kwa moyo mkunjufu watanzania waliojitokeza katika kumsaidia kwa hali na mali mpaka kufanikiwa kupata hela tayari kwa matibabu anayotarajia kwenda kuyapata nchini India.
Cecilia amesafiri kuelekea katika hospitali iitwayo Fortis inayopatikana New Delhi -India kwa matibabu, jumatatu ya tarehe 26 mwezi septemba mwaka huu.
Aidha walezi wa Sesilia familia ya mzee Kambaliko inatoa shukrani zake za dhati kwa watu wote waliojitolea kwa moyo kumsaidia binti yao kwa kutoa pesa, mavazi na hata waliowapa maneno ya faraja pamoja na wale wote wanaoikumbuka familia hiyo katika maombi.
Kabla ya safari yake hiyo, hali ya kiafya ya sesilia ilikuwa ikiendelea vizuri, kwani alikuwa anaweza kupumua na kukaa, tofauti na awali kutokana na kupunguzwa kwa kiasi cha maji katika tumbo lake hospitalini Regency alipolazwa kwa ajili ya matayarisho kabla ya kuanza safari yake kuelekea nchini India kwa matibabu zaidi.
Mtoto huyu aliondoka hapa nchini jumatatu ya tarehe 26 na ndege ya shirika la Quatar Airways akifuatana na daktari mmoja kutoka hospitali ya regency, pamoja na mlezi mmoja mpaka nchini India alipotarajia kupokelewa na madaktari tayari kwa uchunguzi wa kina na kisha kuanza matibabu yake.
Kipindi cha Mimi na Tanzania kinapenda kuwashukuru Watanzania wote pamoja na makampuni mbalimbali yaliyojitolea katika kumsaidia Sesilia kwa ajili ya matibabu. Shukrani za pekee ziifikie hospitali ya regency hasa daktari Kanabar kwa uvumilivu na huduma nzuri kwa Sesilia. Pia kwa mchango wao wa kulipia nauli ya kwenda nchini India kwa Sesilia, mzazi na daktari ikiwa ni pamoja na matibabu ya awali anayoyapata hivi sasa.
Watanzania, pamoja tumeweza tena. Sesilia ni mmoja tu kati ya watoto milioni moja wanaosumbuliwa na tatizo hili, hebu tujitolee kuwasaidia watoto hawa bila ya kuchoka, pia tusimsahau binti huyu kwa maombi ili upasuaji anaotarajia kufanyiwa umalizike salama na kwa mapenzi yake Mungu mtoto huyu arudie katika hali ya kawaida kama watoto wengine. Mungu mbariki Sesilia.Amen!
No comments:
Post a Comment