Na Mwandishi Wetu
BAADA ya Bonanza la kwanza la wadau wa burudani ambao ni kampuni ya Media Entertainment Group kwa kushirikiana na bendi ya Extra Bongo kufana, hatimaye wadau hao wameamua kunogesha ubora wa Bonanza la leo ambalo litakuwa la aina yake.
Mwenyekiti wa Bonanza hilo linalofanyika kila Jumapili kwenye uwanja wa TP, Sinza Uzuri jijini Dar es Salaam, Rachel Mwiligwa alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba tofauti na wiki iliyopita, bonanza la leo limeongezewa burudani kibao, ambapo mbali na kuongezeka kwa timu shiriki, pia kutakuwepo na burudani ya ziada kutoka kwa bendi mbili, za Extra Bongo inayoongozwa na Ally Choki na Bantu Group chini ya Commandoo Hamza Kalala.
Mwiligwa alisema kutokana na kuongezeka kwa timu, wameamua kuweka zawadi ya jezi kwa ajili ya kushindaniwa, ambazo zimetolewa na mdau maarufu anayemiliki maduka ya jezi, Spear Mbwembwe.
Alisema bonanza la leo litakuwa funga kazi kwani pamoja na mechi za ushindani mkali kutoka kwa timu mbalimbali zitakazoshiriki, Extra Bongo na Bantu wameahidi kupagawisha mashabiki mara mbili ya walivyofanya wiki iliyopita.
Mmoja wa viongozi wa bendi hiyo Ramadhani Masanja Banzastone aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba wameahidi kutoa burudani ya ziada ambapo yeye, Ally Choki na Roggart Hegga Katapilla, watapiga nyimbo zao zote walizotunga wakiwa katika bendi mbalimbali.
Kuhusu timu, Mwenyekiti Mwiligwa alisema timu nyingi zimethibitisha kushiriki, ingawa aliwataka washiriki kuwahi kufika kwani Bonanza litaanza kuanzia saa 2:00 asubuhi. Aidha aliwashukuru baadhi ya wadau ambao wamekuwa wakisaidia ufanikishwaji wa Bonanza hilo zikiwemo timu za Wahenga, MSD, Villa, Shein, Uongozi wa baa ya Freetown, Goodluck wa baa ya Meeda, Masoud Wanani, Mzee wa Pamba, Fred Mopao, Nassoro Fundikira na wengineo kibao.
Aidha kutakuwepo na ugeni wa wanamuziki wanaounda kundi la Mapacha Watatu, Kalala Junior, Khalid Chokoraa na Jose Mara ambao watabadilishana mawazo na wadau.
No comments:
Post a Comment