Habari za Punde

*WANANCHI WA MANISPAA YA IRINGA WACHOMA MOTO NYUMBA YA KAKA JAMBAZI

 WANANCHI wa Manispaa ya Iringa wafanikiwa kuvunja na kuteketeza kwa moto nyumba Msafiri Ilomo ambayo ilikuwa ikitumika kama ngome ya ujambazi katika eneo la Kigamboni kata ya Mwangata na kufanikiwa kukuta mali mbali mbali ambazo wananchi walikuwa wakiporwa kabla ya kupigwa nondo .

Pamoja na wananchi hao kuteketeza kwa moto nyumba hiyo na mali mbali mbali zinazodaiwa kuwa ni za wizi bado baadhi yao walionekana wakiiba baadhi ya mali hizo za wizi zilizokuwa zikimilikiwa na jambazi huyo, ambapo walikuwa wakibeba na kuondoka nazo eneo hilo.

Hatua ya wananchi hao kuvunja nyumba hiyo ilikuja baada ya mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi, kufika eneo hilo na kushuhudia wingi wa mali zilizoporwa kwa wananchi zikiwemo mali za baadhi ya wananchi ambao waliuwawa kwa kupigwa nodo na majambazi hao.

Kabla ya Mwamwindi kukubali ombi la wananchi hao la kutaka nyumba hiyo kuvunjwa katika eneo hilo tayari jeshi la polisi lilifika eneo hilo na kusomba mali mbali mbali kwa zaidi ya tripo mbili na kwenda kuzihifadhi kituo cha polisi kwa ajili ya utambuzi zaidi .

Akizungumza na wananchi hao Mwamwindi alisema kuwa kutokana na nyumba hiyo kuwa na alama ya X kutokana na kujengwa bila ruhusa ya ofisi ya Manispaa ya Iringa anaagiza baada ya jeshi la polisi kumaliza kazi yao nyumba hiyo kuvunjwa .

Meya huyo alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa juu ya tukio hilo la ujambazi katika kata ya Mwangata ambapo wananchi walikuwa wakiishi kwa hofu kubwa na tayari watu zaidi ya wawili wamepoteza maisha kwa kupigwa nondo huku baadhi ya wanawake wakiripotiwa kubakwa na kundi hilo la ujambazi lililokuwa na masikani yake Kigamboni katika nyumba ya jambazi huyo Ilomo.

Baadhi ya majeruhi waliopigwa nondo na kukatwa mapanga na kundi hilo la ujambazi akiwemo Michael Chengula (37) aliyevunjwa mkono wake wa kushoto kabla ya kuporwa simu na fedha kiasi cha laki moja na Adilian Lusasi (45) ambaye ni mpiga picha aliyeporwa kamera na picha za wateja wake walisema kuwa walivamiwa na jambazi huyo na kundi lake majira ya saa 3 za usiku zaidi ya wiki tatu zilizopita.

Pia walisema tayari kijana Damas Kisinga amepoteza maisha kwa kupigwa nondo na kundi hilo la ujambazi na kuzikwa juzi katika eneo la Makanyagio huku nyumba ya diwani wa kata ya Mkwawa Thobias Kikula ikivamiwa na wezi hao ambao walishindwa kufanikiwa baada ya kuzingirwa na wananchi .

Diwani wa kata ya Mwangata Galus Lugenge akielezea mali zilizokamatwa alisema kuwa ni pamoja na TV, DVD, nguo, vyombo ,Magodoro , Baiskeli, sofa ,masanduku ya nguo , vitanda , mabati na simu aina mbalimbali,visu , CD , vyombo vya makanisani na misikitini na mali nyingine nyingi ambazo zilijaa nyumba na kusombwa na magari ya polisi.

Alisema kuwa mwezi mmoja uliopita jambazi huyo alifiwa na mtoto wake na kulazimika kuzika kwa siri na msiba kutenga nyumbani kwa mzazi wake akihofu wananchi kujua siri nzito katika nyumba hiyo kuu kuu (Pagale).

Diwani Lugenge alisema kuwa nyumba hiyo ilikuwa haijakamilika japo ilifunikwa kwa trubai pekee na nje alikuwa amefunga dishi la kawaida na la DSTV jambo mbalo liliwafanya wananchi kuishuku nyumba hiyo na kuivamia kabla ya jambazi hilo kufanikiwa kuwatoroka.

 Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Iringa wakishuhudia tukio hilo la kuteketeza moto Nyumba ya Kaka Jambazi huyo.
Huyu ndiye Msafiri Ilomo, mmiliki wa mtandao wa ujambazi ambaye anatafutwa na jeshi la polisi mkoa wa Iringa.
Ilomo, ndie mmiliki wa nyumba iliyokutwa na mali za wizi eneo la Kigomboni mjini Iringa jana, na ndie anayedaiwa kumiliki kundi la wapiga nondo mjini Iringa Kwa yeyote mwenye taarifa ama atayemuona atoe taarifa kwa jeshi la polisi.
Picha na Stori, Francis Godwin Iringa
--




No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.