Meneja Mpya wa Msanii wa Muziki wa Dansi nchini,Charles Baba, Bw. Bernard Msekwa, akisisitiza Jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na kumchukua msanii huyo na kumkabidhi kundi na bendi mpya. Mkutano huo ulifanyika leo mchana kwenye mgahawa wa Hadd's uliopo katikati ya jiji la Dar es Salaam leo.
******************************************
Na Mwandishi Wetu, Jijini Dar
MWIMBAJI wa kutumainiwa wa bendi ya muziki wa dansi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ Charles Gabriel ‘Chaz Baba’ ametangaza kujitoa katika bendi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mchana, msanii huyo alisema kujitoa kwake kumetokana na mambo mengi mojawapo ni kutokuwa na mkataba wa kazi.
Alisema tangu ajiunge na bendi hiyo mwaka 2005 hajawahi kupewa mkataba wowote wa kazi zaidi ya kulipwa mshahara tu kitu ambacho amekiona kama ni kinyume na utaratibu wa kazi.
Aidha Chaz aliongeza kuwa baada ya kujitoa ndani ya bendi hiyo kwa sasa atakuwa akisimamiwa na meneja wake aliyemtaja kwa jina la Benard Msekwa.
“Kwa sasa nitakuwa nasimamiwa na meneja wangu mpya (Msekwa) hivyo kila kitu kinachohusu masuala yangu ya kazi ama ya kisanii kwa ujumla kitakuwa chini yake, kama ni onyesho ama kuhamia bendi nyingine yeyote ni juu yake,”Alisema.
Aidha, nyota huyo aliongeza kuwa baada ya kujitoa Twanga Pepeta huku akisubiri mambo mengine, ataelekeza nguvu zake katika kuandaa albamu yake binafsi itakakuwa na jumla ya nyimbo nane.
“Mpaka sasa nimeshakamilisha vibao kama sita hivi hivyo katika miezi ya karibuni nadhani itakamilika.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni pamoja na Nusu Chizi, aliyowashirikisha Mapacha Watatu, Blandina, Papa Fred, Mayasa na Ninaelekea wapi,”Alisema.
Naye meneja wa msanii huyo, Msekwa alisema kuwa wamekamisha taratibu zinazostahili juu ya kumng’oa Baba Twanga Pepeta ikiwemo kulipa mshahara wa mwezi mmoja.
Kuondoka kwa Charlz Baba kumethibitisha taarifa za kutaka kujiengua kwake, hivyo kufanya bendi hiyo kuendelea kuwa na pengo kutokana na wasanii kadhaa kuondoka katika siku za hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment