Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr. Shukuru Kawambwa (MB) akimkabidhi Sheria ya Mfuko wa Elimu Mwenyekiti wa bodi mpya ya Mamlaka ya Elimu Tanzania Dkt Naomi Katunzi mara baada ya kuizindua bodi hiyo.
Wajumbe wa bodi mpya ya Mamlaka ya Elimu Tanzania katika picha ya pamoja na mgeni rasmi. Waliokaa kutoka kushoto ni Profesa Imannuel Bavu, katibu wa bodi hiyo na mkurugenzi wa mamlaka Rosemary Lulabuka, Mgeni rasmi aliyezindua bodi hii Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr. Shukuru Kawambwa (MB), Mwenyekiti wa bodi Dkt Naomi Katunzi na Profesa Siriel N. Massawe. Waliosimama kutoka kushoto ni Vuai Khamisi Juma, na Ndugu Kalinga.
*************************************
MAMLAKA YA ELIMU TANZANIA YAZINDUA BODI RASMI
Akiongea katika hafla hiyo mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa(MB) amesema Mamlaka ya Elimu Tanzania ni taasisi muhimu na inategemewa kwa kiasi kikubwa na wadau wengi wa elimu hivyo aliwashukuru wajumbe wote kwa kukubali kwao uteuzi huo.
Waziri Kawambwa akaongeza kuwa Mamlaka ya Elimu Tanzania ina majukumu mengi kulingana na Sheria Namba 8 ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001 na akayaanisha majukumu makuu kuwa ni pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu na Kuratibu matumizi ya rasimali hizo kwa ajili ya kufadhili miradi ya elimu.
Aidha Waziri kawambwa alisisitiza kuwa “Mamlaka ya Elimu Tanzania imefanya kazi kubwa katika kuongeza ubora wa elimu na kuongeza upatikanaji wake kwa usawa. Nina taarifa kuwa miradi ambayo tayari imefadhiliwa na kuratibiwa kwa ufanisi mkubwa ni miradi 1,290 yenye thamani ya TShs.36.7 billioni hii si kazi ndogo ndugu zanguni na inahitaji pongezi kubwa”.
Naye mwenyekiti wa bodi Mamlaka ya Elimu Tanzania Dkt Naomi Katunzi amesema wako tayari kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kwa weledi ili kuhakikisha Mamlaka inafikia malengo yake. Ikiwemo kuhakikisha sheria ya Mfuko wa Elimu inarekebishwa ili kuanisha vyanzo vya mapato endelevu na vya uhakika.
“Changamoto kubwa ndani ya Mamlaka ni kuhakikisha kuwa inakuwa na vyanzo vya mapato endelevu, sasa moja ya kazi ya Bodi hii itakuwa ni kuishauri Serikali juu ya vyanzo mbalimbali vya uhakika vya mapato kwa ajili ya Mfuko kisheria” Alisema Dkt Katunzi.
Aidha bi Katunzi ameongeza kuwa baadhi ya maeneo yatakayoshughulikiwa na Mamlaka chini ya bodi hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kusadia kupunguza tatizo la matundu ya vyoo kwa shule za msingi, kupunguza tatizo la madawati , Kujenga mabweni, kujenga maktaba na kusaidia vifaa vya teknohama.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilianzishwa kwa sheria ya Bunge Na. 8 ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001, kifungu cha 5(1) ikiwa na jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu. Majukumu Makubwa ya Mamlaka ya Elimu ni pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu na kufadhili miradi mbalimbali ya elimu katika ngazi zote za elimu nchini.
Bibi . Sylvia Lupembe Gunze
Meneja Habari Elimu na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment