Habari za Punde

*BAADA YA MTAFARUKU KLABU YA SIMBA, KOCHA MILOVAN AWAASA SIMBA KUHUSU BOBAN


ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, ameutaka uongozi wa timu hiyo kuhakikisha unamrudisha na kumbakiza kundini kiungo wake aliyesimamishwa, Haruna Moshi ‘Boban’. 
Boban pamoja na beki wa timu hiyo Juma Nyoso, walisimamishwa hivi karibuni na uongozi wa timu hiyo kutokana na kile kilichodaiwa utovu wa nidhamu. 
Akizungumza na mtandao huu, Kiongozi mmoja wa Simba, alisema kuwa  Milovan alitoa wosia huo muda mfupi kabla ya kuondoa nchini kutimkia kwao Serbia  kwa mapumziko na kusema kwamba, Boban ni mchezaji mzuri hivyo Simba kama itamtosa moja kwa moja itakuwa imepoteza lulu. 

Milovan, alisema kuwa hakuna mchezaji kama Boban, katika ukanda wa Afrika Mashariki na hilo alilibaini kupitia michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame iliyofanyika nchini mwezi Agosti na Yanga kutwaa ubingwa . 
“Kocha alituambia kuwa hata kama tutaamua kuachana naye yeye, lakini tusimuache Boban, kwani ni mchezaji mzuri na kasoro alizonazo ni za kibinadamu tu, kikubwa ni uongozi kutochoka kwa kumjenga kisaikolojia tu,”alisema kiongozi huyo, ambaye hakupenda jina lake kuandikwa. 
Tayari uongozi wa Simba umeshawapa barua za kuwataka wachezaji hao kujieleza na baadaye Uongozi utatoa maamuzi dhidi yao. 

Hata hivyo wakati Uongozi ukitoa barua na kuda kwa wachezaji hao kujieleza,  taarifa kuna taarifa zilizozagaa kuwa tayari Beki wa timu hiyo, Juma Nyoso, ameshapelekwa kwa mkopo katika timu ya Coastal Union ya Tanga huku Boban akitarajiwa kurejeshwa kundini si tu kwa ajili ya uwezo alionao bali kukingiwa kifua na baadhi ya watu wenye nguvu ndani ya klabu hiyo.

Uongozi wa Simba ambao kwa sasa upo katika shinikizo la kutakiwa kujiuzulu na wanachama kutokana na mwenendo mbaya wa timu kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uliomalizika kwa timu hiyo kushika nafasi ya tatu nyuma ya Azam Fc na Yanga inayoongoza,  utakutanana wakati wowote kujadili suala hilo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.