Azam ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga ndizo zitakazoumana kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 itakayochezwa kesho jioni (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Timu hizo zimepata fursa hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali ya michuano hiyo inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom. Michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai.
Azam ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata tiketi ya fainali baada ya kuitoa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa mikwaju ya penalti 3-2. Matokeo ya dakika 90 yalikuwa bao 1-1. Nayo Coastal Union iliivua ubingwa Simba kwa kuifunga mabao 2-1.
Mechi ya fainali itaanza saa 10 kamili jioni, na itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Mtibwa Sugar na Simba ambayo itachezwa saa 2 kamili asubuhi kwenye uwanja huo huo.
Mbali ya kombe, bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, makamu bingwa sh. milioni 1 wakati mshindi wa tatu atajinyakulia sh. 500,000. Timu iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh. 300,000.
Naye kocha bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa bora.
No comments:
Post a Comment