Habari za Punde

*AZAM ILIVYOILAMBISHA ICE CREAM SIMBA NA KUTINGA FAINALI ZA KOMBE LA MAPINDUZI JANA USIKU

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

AZAM FC, jana usiku imetinga Fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuichapa Simba SC kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 ndani ya dakika 120 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Amani, mjini Zanzibar.

Hadi mapumziko, Azam FC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na kiungo Mkenya, Humphrey Mieno, katika dakika ya 10, baada ya kuunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na kiungo mzalendo, Ibrahim Mwaipopo.

Aidha mchezo huo, uliingia dosari pale uliposimama kwa muda wa dakika 5, hadi ulipoanza katika dakika ya 19 kutokana na kukatika kwa umeme  uwanjani hapo, hali iliyolazimisha kuwashwa kwa Jenereta.

Kipindi cha pili Simba walibadilika kiuchezaji na kuanza kutawala mchezo jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 78, bao lililofungwa na Rashid Ismail.

Simba ilipoteza nafasi mbili za wazi katika dakika 45 za kipindi cha pili na mchezo ukamalizika timu hizo zikiwa sare kwa kufungana bao  1-1.

Katika dakika 30 za nyongeza, Simba walifanikiwa kupata bao lililoelekea kuwa la ushindi katika dakika ya 110, lililofungwa na Miraj Madenge.

Azam walionekana kuchanganyikiwa zaidi na kucheza kwa kasi na uwezo zaidi baada ya kufungwa bao hilo la pili huku wakionekana kucheza rafu zaidi na kusababisha wachezaji wake wawili Mwaipopo na Jabir Aziz, kupewa  kadi nyekundu.

  
Wakati refa huyo akijiandaa kupuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo na mashabiki wa Simba wakiwa wameuteka Uwanja wa Amani kwa shangwe zao, beki Emily Mgeta alimuangusha kwenye eneo la hatari beki Malika Ndeule na hivyo kuwa adhabu ya penalti.

Beki Mkenya, Joackins Atudo ambaye amekuwa akipewa dhamana ya kupiga penalti kwa sasa Azam FC, alikwenda kupiga mkwaju huo na kuukwamisha nyavuni kuwapatia Watoto wa Bakhresa bao la kusawazisha.

Kwa matokeo hayo sasa, Azam itamenyana na mshindi wa kesho kati ya Tusker na Miembeni katika fainali Jumamosi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.