Habari za Punde

*HABARI KUTOA IKULU ZANZIBAR


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar
       20 April, 2013
________________________________________
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein amezitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kushirikiana na
vyombo vya Ulinzi na Usalama kudhibiti wimbi la wizi wa mazao na
mifugo lililoshika kasi Zanzibar hivi sasa.
Dk. Shein amesema suala hilo lazima lishughuklikiwe vizuri na kwa
umakini mkubwa kwa sababu hatua iliyofikiwa sasa na vitendo vya baadhi
ya wezi kukata sehemu za viungo vya mifugo kama ng’ombe na kuwaacha
wazima sio tu kuwa ni ukatili lakini ni  vitendo ambavyo haviwezi
kufikiriwa kufanywa Zanzibar.
Rais ametoa wito huo wakati akihitimisha majadiliano ya Mkutano wa
Tathmini ya Taarifa ya Utekelezaji Mpangokazi wa Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Idara ya Uratibu Mamlaka za Mikoa na
Serikali za Mitaa uliofanyika jana Ikulu.
“Ni vitendo vibaya na vya kikatili kukata baadhi ya viungo vya mnyama
bila kuchinjwa huku ukimwacha akihangaika kwa maumivu.Lazima tuwe
makini na hatua za kuchukua kwa kuwa wanaofanya vitendo hivi  si watu
wa kawaida” alisema Rais na kueleza hofu yake kuwa nyama hiyo huishia
kuuzwa kwa matumizi mbalimbali ya wananchi kitendo ambacho kinaingilia
hata imani ya dini.
Sambamba na agizo hilo Dk. Shein amewakumbusha viongozi na watendaji
wa mamlaka hizo kuelewa kuwa mamlaka hizo ndizo zilizo karibu na jamii
na ndizo zinazoshughulikia masuala ya wananchi hivyo kila wakati wawe
tayari kupokea na kutafuta njia za kukabiliana na changamoto
mbalimbali kutoka kwa wananchi hao.
“Huko mliko ndiko kwenye wananchi… sisi wote humu(kikaoni) tunaishi
katika maeneo ya mamlaka zenu hivyo hoja zitakuja, malalamiko yatakuja
na hata pongezi wakati mwingine wananchi watakujanazo zote tuzipokee”
Dk Shein alisisitiza.
Aliwasisitizia washiriki wa mkutano huo wakiwemo wakuu wa Mikoa na
Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Watendaji wa
Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri kuwa ni wajibu wao kujibu
hoja za wananchi kwa kadri wanavyozielewa na kwa kufuata Sheria na
taratibu zinazowaongoza.
Rais alieleza kuridhishwa kwake na mwelekeo mzuri wa ukusanyaji mapato
katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuzitaka ziongeze
jitihada zaidi ili zifikie hatua nzuri ya kupunguza utegemezi wa
ruzuku na hatimae ziweze kujitegemea.
“Tuongeze kasi ya utekelezaji majukumu yetu kwa kuongeza  kasi ya
ushirikiano, kasi ya mashauriano na kupunguza kasi ya kulaumiana na
tukubali tujisahihisha pale tunapokosolewa”aliwasisitizia viongozi na
watendaji mamlaka hizo.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharriff Hamad
ametoa wito kwa watendaji wa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa
kuhakikisha wanakuwa makini katika matumizi ya fedha za makusanyo
katika mamlaka zao.
Akichangia katika mjadala huo Maalim Seif amesema mwelekeo mzuri wa
makusanyo ya fedha katika mamlaka hizo ni ishara ya mwitikio mzuri wa
wananchi kulipa kodi mbalimbali hivyo matokeo mazuri ya matumizi ya
fedha hizo katika utoaji huduma yatakuwa kichocheo zaidi kwao
kuendelea kulipa kodi kama itakiwavyo.
“Nimetiwa moyo na hatua ya ukusanyaji mapato katika Manispaa, Mabaraza
ya Miji na Halmashauri hivyo lazima watendaji wawe makini katika
matumizi ya fedha hizo kwani mapato yanapokuwa mazuri wananchi
wanatarajia huduma nzuri kutokana ma matumizi ya fedha zao” alieleza
Maalim Seif.
Makamu wa Kwanza wa Rais alizungumzia pia kuhusu vitendo vya wizi wa
mazao vinavyoendelea hivi sasa Unguja na Pemba na kueleza kuwa vitendo
hivyo vikiendelea vinavyoweza kuwavunja moyo wakulima hivyo alizitaka
Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa ziongeze jitihada za kukabiliana
nazo.

Postal Address: 2422 Tel.:0776 613 015. Fax: 024 2231822

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.