Katika mahojiano yake na Tido Mhando wa BBC; alisema hivi:
Tido: Wakati wa uteuzi wa chama, Rais Mkapa alitoa hotuba ambayo wengi walidhani alikuwa anakupigia debe wewe. Je, hili lilikushangaza hata wewe binafsi?
Kikwete: Yaani wewe kweli mimi nitashinda kwa hotuba ya jukwaani pale. Ndugu yangu, nilishinda kwa jitihada kubwa ambazo niliziweka mimi na marafiki zangu. Ukweli ni kwamba ilituchukua muda kujijenga. Tulitengeneza mtandao wa watu nchi nzima wa watu wanaotuunga mkono. Tulifanya juhudi kubwa ya kuzungumza na wana-CCM.
Tido: Lakini wakati kiongozi mkubwa kabisa, anapokuja mbele ya wajumbe na kutoa matamshi ambayo yanaonyesha dhahiri yanaelekeza kwamba yeye anamuunga mkono fulani, na ilijihidhirisha hata katika mkutano ule pale watu walipoanza heka heka za Kikwete…Kikwete moja kwa moja.
Kikwete: Mimi sijui ni kupigiwa debe kwa vipi hasa. Hotuba ya Rais, yeye alichokuwa akizungumza tu ni kwamba... Mimi nadhani hotuba yake ilikuwa inasisitiza kwamba; kwanza alichokisema kwamba moja; CCM kama CCM, tuchague watu, lakini tusisahau huyu tunayemchagua sasa, hatimaye tutampeleka kwa watu.
Na huko kwa watu, ni lazima sisi kama chama, kama tunataka kushinda, ni lazima tutambue matarajio ya watu.
Kwa sababu haiwezekani muwe mmekaa tu pale kwenye mkutano, mkajifanya kama vile mmefunga masikio, yaani mmeziba masikio, na macho mmeyaziba, hamuoni na wala hamsikii huko mnakotoka wanasema nini.
Lakini pia, hata wale wanakuja kwenye Mkutano Mkuu wanatoka katika kila wilaya ya nchi yetu.
Ni vizuri kwao wakaangalia matumaini ya watu, na muangalie matumaini ya wale mnaowategemea watakwenda kupiga kura.
Sasa, sina hakika kama kwa kusema hivyo alikuwa na maana yangu mimi!
Tido: Kulikuwa na vitu vingi pale. Oh, mchague mtu ambaye amekulia kwenye chama hiki, anayekifahamu vizuri sana . Ukiangalia kwa undani, ukilinganisha na wagombea wenzako uliokuwa nao pale, sifa zote hizo zilikuwa zimeiva kwako.
Kikwete: Lakini, niseme. Hivi, hivi ni mwana-CCM gani, atateua mtu ambaye hana historia na hicho chama. Hata kama utataka kunilaumu kwa hilo , bado nitaendelea kusema si kweli.
Tido: Hapana si kwamba tunakulaumu, lakini tunasema alionyesha wazi kwamba chama kimchague Kikwete.
Kikwete: Mimi sijui bwana, sijui. Mimi ningependa kuamini kwamba nilifanya jitihada kubwa kushinda, na wasije wakafika mahali wakarahisisha mitihani niliyoipitia. Nilifanya jitihada kubwa sana .
Sisi ni katika wale tunaoamini kwamba mwisho wa uchaguzi mmoja, ni mwanzo wa uchaguzi mwingine. Sisi tulianza mwaka 1995, tukaweka mkakati wa mwaka 2005.Nilifanya kazi kubwa kujenga mtandao. Nilifika mahali, kila mahali ukinitajia Ngara yuko nani, nakwambia yuko fulani.
Nikawa nawajua watu kwa majina. Nimefanya kazi kubwa sana . Ndiyo, nakiri kwamba uzoefu wangu nao katika chama ulinirahisishia. Kwamba hawa watu ninawafahamu, nimeshaishi nao, ndiyo msingi ambao mimi ninadhani umesaidia.
Lakini wanaodhani nilishinda kwa hotuba ya Rais wanatafuta kurahisisha tu ili ionekane kwamba kama isingekuwa hotuba ile watu wasingenichagua. Hata kidogo! Mimi nilianza zamani.
Ninaamini tu kwamba nilifanya jitihada mimi mwenyewe ya kuwaomba wana-CCM waniunge mkono, na ninashukuru walinikubali baada ya kuwaeleza nia yangu ni nini.
No comments:
Post a Comment