Na Mwandishi Wetu
MSANII nguli wa muziki wa dansi nchini aliyetangaza kuachana na kazi ya muziki siku za hivi karibuni, Muhidini Gurumo, leo anatarajia kupanda jukwaani kutoa burudani sambamba na mkewe kwa ajili ya onyesho maalum la kutunukiwa zawadi za heshima.
Gurumo atatoa burudani hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwaaga mashabiki wake na bendi yake ya Msondo, ambapo shughuli hiyo itaambatana na uzinduzi wa kundi la Cash Money lenye Maskani yake Tandika jijini Dar es Salaam.
"Tumeandaa zawadi kwa mzee Gurumo kutokana na heshima kubwa aliyonayo
katika tasnia ya muziki na kujenga maadili kwa taifa kutokana na nyimbo zake.
Hivyo zawadi zetu zitaenda sambamba na uzinduzi wa kikundi chetu cha Cash Money, ili kumbukumbu kubwa kwetu nasi pia tuweze kufika mbali kimalengo katika kazi zetu kama alivyofika mzee wetu Gurumo''. alisema Mlezi wa Kikundi hicho, Latifa Masasi
Uzinduzi huo unafanyika leo jioni kwenye ukumbi wa Equator Grill, Mtoni kwa Aziz Ali, Dar es Salaam na utapambwa na bendi mbalimbali za taarabu zikiwemo Coast na G Five.
Kundi la Cash Money ambalo lilianzishwa mwaka 2011, pia limetoa vitu
mbalimbali kwa wodi ya watoto, na vituo vya watoto yatima jana, ikiwa
ni sehemu ya sherehe na shambra shambra za uzinduzi huo.
No comments:
Post a Comment