Mtafiti toka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu NIMR kituo cha Muhimbili Dkt.
Godfather Kimaro akitoa wito kwa wanchi kujitokeza kwa aajili ya kupima afya
zao mara tu wanapoona dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu ili kupunguza maambukizi
mapya. Katikati ni Mkurugenzi wa NIMR kituo cha Muhimbili Dkt Godfrey Mfinanga
na wa mwisho kulia ni Afisa habari Idara ya Habari MAELEZO Frank Mvungi.
************************************************
Frank Mvungi-Maelezo
Serikali yaendelea kuimarisha Tafiti za kifua kikuu
hapa nchini kwa kushirikiana na Taasisi
za Kimataifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
kituo cha Muhimbili Dkt.Godfrey Mfinanga wakati wa mkutano na waandishi wa
Habari leo jijini Dar es salaam.
Akieleza Dkt.Mfinanga alisema kuwa NIMR kituo cha
Muhimbili imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika tafiti kwa kushirikiana na
Taasisi za kimataifa kama African Research Consortium for Ecosystem and
Population Health (AFRIQUE ONE CONSORTIUM) na East African Consortium for
Clinical Research ( EACCR).
Dkt Mfinanga alibainisha kuwa wastani wa wagonjwa 295 kati ya watu 100,000 hugundulika kuwa na TB ,ambapo Tanzania bara
ilionekana kuwa na wagonjwa wengi zaidi kuliko Tanzania Visiwani,Vijijini
kuliko mijini,watu wazima kuliko vijana,ambapo utafiti huo uko hatua za mwisho.
Akifafanua zaidi amesema tafiti zimeonyesha kuwa kwa
wastani wa asilimia 35 ya wagonjwa wa TB huchelewa kugundulika kutokana na uelewa mdogo na tabia ya wananchi
walio wengi kuchelewa kwenda Hosipitali.
Dkt Mfinanga alitaja maeneo yanayoathiriwa na Ugonjwa wa
kifua kikuu kuwa ni mapafu ,tezi,tumbo,figo, na hata ubongo ikiwa mgonjwa
hatapata matibabu kwa wakati muafaka.
Katika hatua nyingine Dkt Mfinanga amesema kuwa NIMR kituo cha Muhimbili imefanya utafiti
ambao umethibitisha kuwa kuna umuhimu wa
kushirikisha jamii katika kusimamia matibabu ya wagonjwa wa TB (Community
DOT-PCT).
Kufuatia utafiti huo Serikali ilianzisha mfumo huo
ambao umeonyesha mafanikio makubwa kwa kuwa mgonjwa anachagua mahali pa kumezea
dawa za TB kati ya nyumbani akisimamiwa na ndugu au kwenye kituo cha tiba
akisimamiwa na mtoa huduma wa afya.
Naye mtafiti toka NIMR kituo cha Muhimbili Dkt.
Godfather Kimaro alitoa wito kwa
wananchi kuwahi hosipitali pale wanapoona dalili za ugonjwa wa Tb ambazo baadhi
yake ni kikohozi kwa muda wa wiki mbili,homa za mara kwa mara na kukonda.
Kituo cha Utafiti cha Muhimbili (NIMR Muhimbili Centre) ni moja ya vituo nane vya
Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Muhimbili
kilirithiwa kutoka lililokuwa Baraza la Afrika ya Mashariki mwaka 1980 wakati
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu ilipoanzaishwa kwa sheria
ya Bunge Namba 23 ya mwaka 1979.
No comments:
Post a Comment