Kikosi
cha Uchukuzi SC kabla ya mechi na Ukaguzi.
Benchi la timu ya Uchukuzi SC wakiwa wanafuatilia
mchezo dhidi yao na Ukaguzi.
Mkuu wa benchi la ufundi la timu ya soka ya Uchukuzi SC, Kenneth Mwaisabula
Wachezaji wa timu mbalimbali za Uchukuzi SC
wakishangia mara baada ya mchezo
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya soka ya Uchukuzi SC
imeng’ara kwa kuifunga Ukaguzi mabao 3-1 katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea
kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Uchukuzi SC ambayo chini ya benchi
la ufundi mahiri linaloongozwa na Kenneth Mwaisabula ‘Mzazi’ ambaye ni Mkuu wa
benchi hilo, huku Elutery Muholeli
ni kocha na Robert Damian ni meneja wa timu hiyo, waliwapeleka puta wapinzani
wao na kuandika bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Kado Nyoni, baada ya
kuwahi mpira wa kona safi iliyochongwa na Omar Said ‘Chidi’ katika dakika ya
34.
Hatahivyo,
Ukaguzi walisawazisha katika dakika ya 50 kupitia kwa Ben Chezue aliyepiga
mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja golini. Chezue aliingia dakika
49 kuchukua nafasi ya Deo Masanja
aliyekuwa ameumia.
Uchukuzi SC iliongeza bao katika dakika ya 72 lililofungwa Issac Ibrahim aliyeachia shuti kali, lililomshinda kipa wa Ukaguzi, Shomari Dumba.
Nahodha wa Uchukuzi SC, Francis Charles alipigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao la tatu katika dakika ya 90 kwa njia ya penati baada ya Bilal Mleli kushika mpira katika eneo la hatari.
Uchukuzi SC iliyokuwa ikicheza kwa kuonana, awali timu Uchukuzi SC ilikosa magoli kibao ya wazi, baada ya wachezaji wake Abubakar Mwamonchi katika dakika ya 25 kupiga mpira uliopita pembeni kidogo ya goli, huku Francis alishindwa kuunganisha krosi ya Masoud Juma katika dakika ya 30, tena Francis aliyeisumbua ngome ya Ukaguzi katika dakika ya 58 alipaisha mpira akiwa karibu na kipa.
Akizungumza mara baada ya mechi, kocha Muholeli alisema Ukaguzi ni moja ya timu ngumu, lakini aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutoka na ushindi mnono, ambao umesaidia kusafisha njia.
“Hapa tumekuja kushindana na kila mechi kwetu tunaiita ni fainali, hivyo timu zote zilizokuja hapa ni nzuri, ila tunataka tushinde mechi zote ili tujiweke pazuri kushinda na kutwaa kombe hili, kwani tumeshafika fainali mara nne,” alisema Muholeli.
Naye Mwenyekiti wa Uchukuzi SC, Mohamed Ally alisema wamekuja Dodoma kuchukua ubingwa na anauhakika wa timu yake itafanya vyema kutokana na nidhamu ya mazoezi wanayofanya kila siku.
Kikosi cha ushindi cha Uchukuzi SC ni: Barton Willy, Ally Poloto, Omar Said ‘Chidi’, Godwin Ponda, Kado Nyoni, Fidelis Kyangu, Seleman Kaitaba/Issac Ibrahim (63), Francis Charles, Ramadhani Madebe, Abubakar Mwamachi/Omar Kitambo (35), na Masoud Juma/Michael Bernad (46).
No comments:
Post a Comment