Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa
akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni kumi kutoka kwa katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Aziz Mlima wakati wa uchangiaji wa
waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Ubalozi wa
China,makampuni ya China na wananchi wa china akikabidhi mfano wa hundi ya
milioni mia moja kwa Waziri Mkuu
Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa wakati wa uchangiaji wa waathirika wa tetemeko
mkoani Kagera.Wengine Pichani ni Waziri
wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Bw.Charles Mwaijage na Naibu Waziri Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi.Suzan Kolimba.
Naibu Waziri Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi.Suzan Kolimba akizungumza kabla
hajamkaribisha Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa kuzungumza na
wafanyabiashara na mabalozi wakati wa
uchangiaji wa waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar
es Salaam.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa
Majaliwa akiagana na Mwenyekiti wa Taasisi za Sekta Binafsi (TPSF), Bw.Reginald
Mengi baada ya kumalizika kwa harambee ya uchangiaji wa waathirika wa tetemeko
mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.Mwenyekiti uyo alichangia
shilingi milioni mia moja na kumi.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa
akizungumza na Wafanyabiashara na Mabalozi (hawapo pichani) wakati wa
uchangiaji wa waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar
es Salaam.

Mabalozi na wafanyabiashara mbalimbali
wakimskiliza Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo Pichani) wakati
wa uchangiaji wa waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini
Dar es Salaam.
***********************************************
Na Sheila Simba, MAELEZO
Jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimechangwa
na mabalozi na wafanyabiashara kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la
ardhi lililotokea Mkoani Kagera.
Michango hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam katika harambee iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa na kufanyika Ikulu.
Akizungumza katika harambee hiyo Waziri
Mkuu alisema jumla ya nyumba 840 zimebomoka na kuharibika kabisa, wakati nyumba
1264 zimepata hitilafu na zinaweza kufanyiwa marekebisho ili watu waendelee
kuishi katika nyumba hizo.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa shule 4 za
sekondari ambazo ni Nyakato, Ihungo, Kashange na Buhembe zimeharibika na mbili
kati ya hizo yaani Ihungo na Nyakato zimefungwa
kutokana na kuharibika sana.
Madhara mengine yaliyosababishwa na
tetemeko hilo kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni kuharibika kwa vituo vya afya,
miundombinu ya barabara, umeme na njia za mawasiliano na kufanya athari za
tetemeko kuwa kubwa.
Kutokana na athari hizo Waziri Mkuu
amewaomba mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kusaidia waathirika
kwani ni tukio ambalo halikutarajiwa na limeleta hasara kubwa kwa wanakagera na
Taifa kwa ujumla.
“Licha ya michango hii ninayowaomba leo,
tutaandaa safari kwa anayehitaji kwenda kujionea hali halisi ili aone ni namna
gani atakavyosaidia,”alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa
imefunguliwa akaunti ya kuchangia katika maafa hayo kwenye benki ya CRDB
inayojulikana kama KAMATI MAAFA KAGERA akaunti namba 0152225617300 na swift
code ambayo ni CORUtztz na kuwaomba wananchi na watu wengine kutumia akaunti
hiyo kwa kusudi hilo.
Majaliwa amesema pia kuwa utaratibu
unaandaliwa ili kuwawezesha watu kuchangia kwa njia ya Mpesa, tigopesa na
Airtelmoney. Utaratibu huo utakapokuwa tayari utatangazwa ili kuwarahisishia
watumiaji wa mitandao hiyo kuchangia.
Katika harambee hiyo wafanyabiashara
waliochangia ni Mwenyeki Mtendaji wa kampuni za IPP Dkt Reginald Mengi
aliyechangia Tsh million 110, Mohamed Dewji ametoa milioni 100, Subash Patel milioni
150 na Salim Turki aliyetoa mifuko 5000 ya saruji na mabati 3000.
Wengine waliochangia ni kampuni mbali mbali
zikiwemo kampuni ya bia ya Serengeti iliyotoa mifuko 800 ya saruji, Sahara
Tanzania wametoa shilingi milioni 20, Camel Oil kupitia Camel Cement wametoa
mifuko 1000 ya saruji ,Puma wamechangia shilingi million 50, Pepsi Cola wametoa
milioni 50 na Azania Group wamechangia milioni 50.
Baadhi ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa
nchini waliochangia ni pamoja na ubalozi wa China shilingi milioni 100 na
kupeleka madaktari,dawa,mahema na vifaa vingine kwa ajili ya kusaidia waliopatwa
na maafa hayo.
Kuwait kupita ubalozi wao nchini wamechangi
dola elfu 10 za Kimarekani na euro elfu
10, na Nchi ya Kenya iliyopeleka msaada wa mahema,magodoro na dawa.
Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa
Afrika Mashariki wametoa milioni 10, mwakilishi wa China Merchantile Group
ametoa milioni 100, Toyota Tanzania milioni 10, Kamal Group milioni 50, Urban
Group milioni 20, TBL milioni 100, IPTL 50, Tanzania Agriculturak Processing
Zone milioni 30, Umoja wa wafanya biashara ya mafuta ya rejereja milioni 250 na
Group Six wametoa tani 80 za saruji.
Wengine waliochangia ni pamoja Jambo
plastic milioni 20, Tanga Cement mifuko 1000 ya saruji, Agusta Tz milioni 10, Oryx
milioni 50, Kagera Sugar milioni 100 na tani 10 za sukari, Tipper milioni 20
ambapo GBP, Oilcom na Moil watajenga shule mbili zilizoharibika.
Uchangiaji huo umejumuisha pia na watu binafsi
ambao ni wakili wa kujitegemea, Bwana Protase Ishengoma milioni 5 na Melisa
Kataraiya milioni 20.
Tetemeko hilo la ardhi ni kubwa kuliko yote
ambayo yamewahi kutokea hapa nchini na hadi sasa limesababisha vifo vya watu 17
na kuharibu nyumba, majengo na miundombinu mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment