Mbunge wa Kasulu vijijini Mhe
Augustine Vuma (Kushoto) akitoa maelezo
kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January
Makamba wakati viongozi hao
walipotembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
(Katikati ni Bw. Peter Bulugu Kaimu Mkuu wa Kambi - Nyarugusu
Sehemu ya wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba (hayupo pichani) mara baada ya kutembelea kutembelea kambi ya Nyarugusu na kutoa maelezo katika sekta ya mazingira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Martin Mkisi wakikagua uharibifu wa mazingira katika msitu wa Makere katika Wilaya ya Kasulu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akihutubia katika Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kagera Nkanda, Wilayani Kasulu
***********************************************
Na Lulu Mussa, Kasulu
Imebainika kuwa ongezeko kubwa la idadi ya
wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu inachangia kwa kiasi kubwa la uharibifu wa
mazingira kwa kuongeza matumizi ya rasilimali za asili.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu Bw. Peter Bulugu wakati wa
kuwasilisha taarifa ya hali mazingira katika kambi hiyo kwa Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe.
January Makamba
Kaimu Mkuu wa
Kambi wa Nyarugusu Bw. Peter Bulugu amesema kuwa hali ya mazingira
katika kambi si nzuri na inakabiliwa na tatizo la uharibufu wa mazingira
kwakuwa wengi wa wakimbizi hao hutumia kuni kama nishati ya kupikia.
Hata hivyo Bw. Bulugu amebainisha kuwa Ofisi
yake imeeanda mkakati wa upandaji miti ili kunusuru maeneo yanayozunguka, na
kwakuanzia jumla ya miche 900,000 imeoteshwa katika vitalu. Pia Kambi
imedhamiria kugawa majiko banifu ambayo yatatumia nishati kidogo na uzalishaji
wa nishati kwa kutumia takataka za mashambani unatarajiwa kuanza mwezi Novemba.
Aidha, mkakati mwingine ni ujenzi wa nyumba
za tofali mbichi na kuezeka kwa mabati badala ya miti ambapo jumla ya nyumba
800 zimekamilika na nyumba 542 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Alisema
Bw. Bulugu
Akiwa katika Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma,
Waziri Makamba ametembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu na kupata fursa ya
kuongea na wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma katika kambi
hiyo.
Waziri Makamba amesema kuwa ni vema uongozi
na mashirika yanayotoa misaada katika kambi hiyo kuandaa mpango mzuri wa namna
ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi ili ujio wao usiathiri watanzania
wanaozunguka kambi ili shughuli zao za uzalishaji mali kila siku ziwe na tija.
Waziri Makamba aliuagiza Ungozi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi kutafuta pesa zaidi ili mpango wa
kugawa majiko banifu uwafikie wakimbizi wote. "Kaya zilizopo hapa ni
30,000 ninyi mnataka kugawa majiko hayo kwa kaya 3000 tu, nashauri muangalie
uwezekano wa kugawa kwa kaya zote" Makamba alisisitiza.
Waziri Makamba pia ameagiza kufanyika kwa
Ukaguzi wa Mazingira (Environment Audit) ndani ya wiki mbili kwakuwa ni takwa
la kisheria. Na kuwataka na kupanda miti kwa wingi. " Pandeni miti ya aina
mbalimbali mfao miti ya matunda, kuni na mbao ili kunusuru mazingira
yetu".
Waziri Makamba pia alitembelea msitu wa
Makere wenye takriban ekari 75,000 ambao kwa upande wa Makere kusini kumekuwa
na uharibufu mkubwa wa mazingira na kuagiza doria za mara kwa mara ili
kudhibiti wananchi wanaofanya kilimo cha kuhamahama, kukata na kuchoma miti pia
kudhibiti ongezeko la mifugo kwa kuiandikisha ili mgogoro uliopo baina ya
hifadhi na wananchi uweze kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga hoja madhubuti.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba hii leo
ameendelea na ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Mikoa 10 hapa nchini
ambapo leo ni siku ya 13. Waziri Makamba pia atatembelea Mkoa wa Tabora.
No comments:
Post a Comment