Habari za Punde

TANZANIA KUNUFAIKA NA DOLA MILIONI 675.6 KUTOKA KOREA

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamisi Shaaban na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Miradi ya Maendeleo, Wizara ya Uchumi na Fedha wa Korea Kusini Bw. Young Joon Yoon wakiwa na hati ya makubaliano ya majadiliano kuhusu miradi ya kipaumbele itakayopata mikopo nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamisi Shaaban (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Korea baada ya kufanya majadiliano na kukubaliana kuhusu miradi itakayopewa kipaumbele cha kupatiwa mikopo nafuu na Serikali ya Korea, majadiliano hayo
Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Miradi ya Maendeleo, Wizara ya Uchumi na Fedha wa Korea Kusini Bw. Young Joon Yoon wakizungumza jambo wakati wa majadiliano (policy dialogue) na Ujumbe wa Tanzania kuhusu miradi itakayopewa kipaumbe cha kupatiwa mikopo nafuu kutoka Serikali ya Korea
Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Miradi ya Maendeleo, Wizara ya Uchumi na Fedha wa Korea Kusini Bw. Young Joon Yoon wakizungumza jambo wakati wa majadiliano (policy dialogue) na Ujumbe wa Tanzania kuhusu miradi itakayopewa kipaumbe cha kupatiwa mikopo nafuu kutoka Serikali ya Korea.
...................................................

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Serikali za Tanzania na Korea zimefanya majadiliano na kukubaliana miradi ya kipaumbele itakayopata mikopo nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini. 
Makubaliano hayo (Aide Memoire) yamebainisha miradi ya kipaumbele itakayoanza tataribu za kupata mikopo nafuu kwa kipindi cha mwaka 2023 na 2024, yametiwa Saini jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamisi Shaaban na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Miradi ya Maendeleo, Wizara ya Uchumi na Fedha ya Korea Kusini Bw. Young Joon Yoon.
Miradi iliyojadiliwa ilitokana na Makubaliano kati ya Serikali hizo mbili yaliyosainiwa mwezi Septemba 2022 ambapo Serikali ya Korea Kusini iliahidi kuipatia Tanzania jumla ya dola za Marekani bilioni 1 kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Bi. Shaaban ameeleza kuwa mpango huo wa miaka miwili (2023-2024), utahusisha miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa chuo cha kisasa cha reli (SGR) utakaogharimu dola za Marekani milioni 75.8, na ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Binguni-Zanzibar wenyethamani ya dola za Marekani milioni 106.
Miradi mingine ni  Uboreshaji na ukarabati wa Hospitali ya Taifa Muhimbili utakaogharimu dola za Marekani milioni 227.3, Ujenzi wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)-kitakachojengwa Dodoma kwa gharama ya dola za Marekani milioni 60, ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo (dola za Marekani 156.5), ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika njia ya kusafirisha umeme ya Kigoma,-Mpanda-Sumbawanga (400KV), na ufadhili wa bajeti ya Serikali, dola za Marekani milioni 50.
Bi. Amina Khamisi Shaaban alisema kuwa pande hizo mbili zimesaini makubaliano (Aide Memoire), na miradi hii itapewa kipaumbele kwa kipindi tajwa na kwamba majadiliano mengine yatafanyika mwakani (2024) ili kukubaliana maeneo mengine ya miradi itakayopatiwa fedha,” alisisitiza Bi. Amina Shaaban.
“Kwa niaba ya serikali ya Tanzania tunatoa shukurani zetu za dhati kwa serikali ya Korea kwa msaada huu mkubwa, ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kukutana kwenye majadiliano mengine kama haya kujadili masuala mengine ya kuendeleza ushirikiano wetu katika khakikisha Dira yetu ya Maendeleo ya 2025 na ile ya Zanzibar 2050 zinafanikiwa kwa ufanisi,” alisema Bi. Amina.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Miradi ya Maendeleo, kutoka Wizara ya Uchumi na Fedha wa Korea, Bw. Young Joon Yoon, amesema kuwa Serikali yake inajivunia uhusiano imara uliopo kati ya nchi hizo mbili na kuahidi kuendelea kusaidia juhudi za serikali za kuwahudumia watu wake kiuchumi na kijamii.
Bw. Yoon alisema kuwa mbali na fedha hizo zilizoahidiwa kutolewa, Serikali ya Korea Kusini kupitia shirika lake la EDCF, iliipatia Tanzania dola za Marekani milioni 223.4 kuanzia mwaka huu 2023 hadi 2025 ili kutekeleza miradi mitatu ikiwemo Mradi wa Kupanua mfumo wa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) awamu ya pili, dola za Marekani milioni 70, Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Kanzidata ya Ardhi unaogharimu dola za Marekani milioni 65 na Mradi wa Kuboresha Mfumo wa Usambazaji  maji Safi na Taka Katika Manispaa ya Iringa wenye thamani ya dola za Marekani milioni 88.4.
Alisema kwamba, hatua inayofuata kwa miradi iliyokubalika ni kufanya upembuzi yakinifu ambao utaanza mwaka huu kwa baadhi ya miradi na mingine itaanza mwakani.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.