Waziri wa Maliasili na utalii, Shamsa Mwangunga, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu matokea ya mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa mkataba wa kudhibiti Biashara ya Kimataifa ya Wanyama na Mimea, (CITES) uliomalizika mwishoni mwa mwezi March, Doha Qatar.
Msemaji wa Wizara ya Maliaili na Utalii, Matiku, akionyesha sehemu ya hifadhi ya Pembe za Ndovu zinazohifadhiwa na Wizara hiyo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika wizarani hapo leo, Waziri wa Wizara hiyo alipokuwa akizungumzia kuhusu matokeo ya baadhi ya mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa mkataba wa kudhibiti Biashara ya Kimataifa ya Wanyama na Mimea, (CITES) uliomalizika mwishoni mwa mwezi March, Doha Qatar.
Na Dennis Luambano, jijini Dar es SalaamWAZIRI wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, amesema watafanya marekebisho muhimu ya kasoro zilizobainishwa katika mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kudhibiti Biashara ya Kimataifa ya Wanyama na Mimiea iliyopo Hatarini Kutoweka (CITES) na kisha watawasilisha tena maombi ya kuuza meno ya tembo yaliyoko kwenye maghala ya Serikali.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati akielezea taarifa ya mkutano huo uliofanyika hivi karibuni katika mji wa Doha nchini Qatar.
“Baadhi ya mambo yatakayofanyiwa kazi ni yale yaliyojitokeza katika mkutano wa 15 wa CITES ni pamoja na kuongeza mikakati ya kudhibiti ujangili wa tembo nchini na kuzidisha juhudi za kuzia meno ya tembo kuingia au kutoka nje ya mipaka yetu.
“Naomba kusisitiza kuwa baada ya kufanya marekebisho hayo, tutawasilisha upya andiko letu katika mkutano ujao wa nchi wanachama wa CITES kwani tunahitaji fedha hizo kwa uhifadhi na maendeleo ya wananchi,” alisema Mwangunga.
Alisema waliwasilisha hoja ambazo zinakubalika katika utaratibu wa CITES lakini upande wa upinzani uliokuwa ukiongozwa na Kenya ulipinga ombi la Tanzania katika mkutano huo pamoja na kukiri kuwa idadi ya tembo waliopo hapa nchini ni kubwa.
Alisema ombi hilo lilipingwa kwa hoja kwamba kulingana na taarifa za vyombo mbalimbali vinavyojihusisha na utekelezaji na uhifadhi wa mkataba wa CITES, meno mengi ya tembo ambayo yanakamatwa na vyombo vya dola katika hususani bara la Asia yameonekana kutokea Tanzania.
“Na kwa maana hiyo ni kwamba kutokana na tathimini ya ya ujumla ya udhibiti wa usafirishaji haramu wa meno ya tembo ndani ya Tanzania haujafikia kiwango kinachokubalika,” alisema Mwangunga.
Katika hatua nyingine, alisema nchi wanachama wa CITES zilihofia kuwa iwapo Tanzania na Zambia zitaruhusiwa kuuza meno ya tembo yaliyoko kwenye maghala yao ambayo kwa ujumla ni tani 111.5 na kasi ya ujangili itaongezeka.
“Tanzania ina tani 89.8 za meno ya tembo na Zambia ina tani 21.7 na kama nchi hizi zingeruhisiwa kuuza basi ujangili ungeongezeka na hii inatokana na imani kuwa kwa kutoa idhini hiyo kungefungua upya milango ya biashara ya meno ya tembo kwa wafanya biashara haramu,” alisema Mwangunga.
Alisema pamoja na hoja kujibiwa vizuri na ujumbe uliohudhuria mkutano huo, bado Tanzania haikukubaliwa kuuza meno ya tembo kutokana na utaratibu wa mkutano wa CITES unaohitaji hoja kuungwa mkono na theluthi mbili za kura.
“Matokeo ya kura kwenye kamati yalikuwa 57 ni ndiyo na 45 ni hapana kwa hoja kuhamisha tembo wa Tanzania na kwa hoja ya kuuza meno ya tembo matokeo ya kura yalikuwa 59 ni ndiyo na 60 ni hapana.
“Hata hivyo, Tanzania ilipokata rufaa kwenye mkutano wa jumla matokeo ya kura yalikuwa ni 55 ni ndiyo na 55 ni hapana,” alisema Mwangunga.
No comments:
Post a Comment