Habari za Punde

*TASWA YAPIGWA TAFU NA TBL KUELEKEA ARUSHA J-MOSI


Na Mwandishi Wetu, Jijini
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imetoa sh. 4, 875,000 kwa timu ya soka ya Waandishi wa Habari za Michezo Nchini (TASWA FC) kwa ajili ya kushiriki katika bonanza la waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha. Fedha hizo zilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa TASWA FC, Majuto Omary katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TBL. Alisema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya usafiri wa kwenda na kurudi, chakula na posho kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo kwa siku zote watakazo kuwa Arusha. Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Meneja Uhusiano wa TBL, Edith Mushi alisema kuwa msaada huo ni moja ya kazi za TBL katika kusaidia jamii na safari hii wameamua kufanya hivyo kwa waandishi wa habari. Mushi alisema kuwa mbali ya msaada kwa jamii, lengo la TBL pia ni kudumisha ushirikiano wa karibu kwa waandishi wa habari ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya michezo na katika sekta nyingine hapa nchini. Alisema kuwa wanaamini kuwa mchango huo utaleta mafanikio kwa timu hiyo na kuweza kutetea vyema taji lake. “TBL inatambua na kuthamini mchango wenu katika maendeleo ya sekta mbali mbali ikiwa pamoja na michezo, tunayo furaha kubwa kuona leo hii mmekuwa mfano wa kuonyesha kwa vitendo mchezo wa soka, tunawatakia kila la kheri katika mashindano hayo na katika kazi ya kuelimisha na kukosa jamii,” alisema Mushi. Mwenyekiti wa TASWA FC, Majuto Omary alishukuru TBL kwa msaada huo mkubwa ambao umeipa nafasi timu yake kutetea ubingwa wake ipasavyo. Majuto alisema kuwa TBL imeonyesha mfano wa kuigwa kwa jamii kwani imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia masuala mbali mbali ya jamii hapa nchini.“Hii ni faraja kuwa kwa TASWA FC kwa kuwa na kampuni yenye kujali waandishi kama TBL, tunaahidi kufanya vyema katika mashindano hayo na kuibuka na ushindi,” alisema Majuto. Alisema kuwa Tanzania kuna makampuni mengi sana, lakini kutokana na kutojua umuhimu wa waandishi wa habari, wameshindwa kuchangia punde waombwapo misaada, na mara nyingi wakitoa majibu ya barua ya maombi kwa njia ya simu siku tatu kabla ya safari ya kuwa ``ombi lenu halikufanikiwa’’. “Kwa kweli tumepata usumbufu mkubwa sana, kwani tulikuna vichwa ili kujua nini kifanyike ili kuikomboa timu na kufanikisha safari yetu,” alisema Majuto.

Meneja Uhusiano wa TBL, Edith Mushi (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi ya thamani ya shilingi milion 4.8, Mwenyekiti wa TASWA Fc, Majuto Omary kwa ajili ya timu hiyo inayoundwa na waandishi wa habari za michezo inayokwenda Jijini Arusha kushiriki mashindao ya Bonanza yanayotarajia kufanyika Agost 1 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Katikati ni Ofisa Uhusiano wa TBL, Lilian Erasmus.


No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.