Habari za Punde

*AJALI YA ROLI YAUA WATATU NA KUJERUHI 37 TARIME

Na Christopher Gamaina, Tarime

WATU watatu wamekufa na wengine 37 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya lori lenye namba za usajili T 905 ALT aina ya Fuso walilokuwa wakisafiria kutoka Tarime mjini kwenda mnadani mji mdogo wa Nyamongo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Constantine Massawe, amewataja waliokufa kuwa ni Paulo Mbonduli (28) na Matiko Range (36) wakazi wa mjini Tarime waliokufa katika eneo la ajili.

Amemtaja mwingine aliyekufa kuwa ni Lucas Matongo (28) mkazi wa kijiji cha Nyansincha aliyefariki dunia mara baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, ambapo miili ya marehemu hao ilihifadhiwa.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Samson Charles, aliliambia gazeti hili kwamba vifo vya watu hao vimesababishwa na kuvunjwa damu nyingi katika majeraha waliyopata sehemu mbalimbali ndani na nje ya miili.

Majeruhi 27 wamelazwa wodi namba sita na saba hospitalini hapo na wengine 10 wamelazwa katika kituo cha afya cha Nyamongo kwa matibabu. Baadhi wamevunjika miguu na kupata majeraha makubwa sehemu za vichwa, mikono, migongo na tumbo.

Kamanda Massawe amewataja baadhi ya majeruhi hao kuwa ni Mariam Mohono (32), Ester Ngoko (28), Nchagwa Chacha (31), Ehelena Paulo (38), Mwajuma Dickson (28) na Anastazia Mwita (28) ambao ni wakazi wa vijiji mbalimbali wilayani Tarime.

Baadhi ya majeruhi wengine ni Olung’a Makopolo (38) aliyevunjika miguu yote miwili, Mwita Chacha (27) aliyevunjika mguu ukabaki eneo la ajali, Magabe Motera (34), Marwa Keng’anya (30), Juma Gimeno (35), Thomas Kerango (41) na Marwa Kesagero (28).

Ajali hiyo ilitokea jana saa 11 alfajili kwenye mteremko wa barabara jirani na uwanja wa ndege wa Mgodi wa Dahabu wa North Mara katika kijiji cha Kewanja baada ya dereva kushindwa kulimudu lori hilo linalodaiwa kukatika breki ghafla.

Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, dereva wa lori hilo aliyefahamika kwa jina moja la Majuto alikimbilia kusikojulikana mara baada ya ajali hiyo kutokea.

Dk. Charles alisema ofisi yake ilikuwa imeandaa magari mawili kwa ajili ya kusafirisha majeruhi walioumia zaidi kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Mwandishi wa habari hizi alifika wodi namba sita na saba ambamo alishuhudia majeruhi wakipatiwa matibabu ya kuongezewa damu na dripu za maji huku baadhi wakiwa wamelala chini na wengine kulala wawili katika kitanda baada ya wodi kuelemewa na idadi kubwa ya majeruhi.

Majeruhi waliozungumza na gazeti hili walisema lori hilo lilikuwa limepakia zaidi ya watu 40 huku likiwa limepakia idadi kubwa ya marobota na mafurushi ya mitumba.

Baadhi ya majeruhi wakiwa wodi ya Hospitali ya Wialaya ya Tarime baada ya kufikisha hapo kufuatia ajali hiyo.
Majeruhi....



No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.