SHIRIKA la Ndege la Precision linalotoa huduma bora
Tanzania, limetangaza kuleta ndege yake mpya ya sita aina
ya ATR42-500 itakayowasili Agosti 26 mwaka huu kutoka
Toulouse, Ufaransa, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza
programu ya kutoa huduma za kisasa zaidi.
Mkurugenzi Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Precision Air,
Alfonse Kioko, aliwaambia waandishi wa habari Dar es
Salaam jana kuwa, ndege hiyo mpya itakayopachikwa jina la
Bukoba, itafuatiwa na nyingine ya saba itakayoingia
Septemba 15 mwaka huu.
Mwaka 2006, Precision na ATR ya Ufaransa walisaini
mkataba wa dola za Marekani milioni 129 ili kutoa ndege
saba mpya. Ndege ya kwanza kati ya hizo iliwasili Machi
2008. Tangu wakati huo, Precision imepokea ndege tano
aina ya ATR 72-500 na kufanya iwe na ndege tano mpya
mpaka sasa. Pia ina ndege nyingine tatu za zamani.
Kioko alisema baada ya ndege hiyo yenye namba 5H-PWF
kuwasili, wataizindua Dar es Salaam Agosti 27. Alisema ina
vifaa vya kisasa vya burudani kwa ajili ya wasafiri kuangalia
sinema na kusikiliza muziki wakiwa safarini. Ndege hiyo ina
uwezo wa kubeba abiria 70.
Mkurugenzi huyo pia alitangaza kwamba tangu kuanza
mwaka mpya wa fedha, idadi ya abiria wapya imeongezeka
kwa asilimia 12 kulinganisha na mwaka jana. Pia mizigo ya
biashara imeongezeka licha ya kudorora kwa uchumi
duniani.
Akizungumza katika mkutano huo, Meneja Masoko wa
Precision, Emillian Rwejuna alisema kampuni hiyo inatarajia
kupata ndege ya Boeing 737, kati ya Oktoba na Novemba
mwaka huu.
Rwejuna alisema kupatikana kwa ndege hiyo kutapanua
wigo wa huduma za safari. Ndege hiyo ya tatu aina ya
Boeing 737 itaboresha safari za Johannesburg, Afrika Kusini,
na pia katika miji ya Kinshasa na Lubumbashi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.
Precision Air hivi sasa inafanya safari katika miji ya Dar es
Salaam, Mwanza, Tabora, Musoma, Shinyanga, Kigoma,
Kilimanjaro, Zanzibar, Mtwara na Arusha. Pia ina safari za
Nairobi na Mombasa, Kenya na Entebbe, Uganda.
No comments:
Post a Comment