Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akiangalia ramani ya mchoro wa jeti inayotaka kujengwa na Hoteli ya Palumbo Reef kutoka kwa mmiliki wa Hoteli hiyo Bwana Palumbo Sila (kulia) wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kujionea maandalizi hayo, leo asubuhi, mjini Zanzibar.
Kibanda cha Hoteli ya Palumbo Reef iliyopo Uroa kinachotarajiwa kuunganishwa na Jeti inayoelekea Baharini kwa ajili ya michezo ya Watalii wa Hoteli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Hoteli ya Palumbo Reef mara baada ya kutembelea eneo linalotaka kujengwa jeti kwa ajili ya wakatii wa Hoteli hiyo. Kati kati yao aliyevaa nguo nyeupe ni mmiliki wa Hoteli hiyo Bwana Palumbo Sila.
************************
Makampuni na Taasisi zinazojihusisha na masuala ya uwekezaji katika Sekta ya Utalii yametakiwa kuzingatia taratibu za tathmini ya kimazingira kabla ya kuanzishakwa miradi yao kwa lengo la kujilinda na uchafuzi wa Mazingira pamoja na rasilmali za Taifa.
Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kutembelea eneo lilalotaka kujengwa Jeti itakayopitisha watalii kwa ajili ya michezo ya Baharini ambalo limelalamikiwa na Idara ya Mazingira Zanzibar kukiuka Taratibu za kimazingira katika Hoteli ya Palumbo Reef iliyopo Uroa Wilaya ya Kati.
Balozi Seif alisema Hoteli au mradi wowote wa kitalii unaotaka kuwekezwa Nchini lazima uzingatie na kukubalika kufanyiwa tathmini ya kimazingira na Taasisi inayohusika na masuala hayo ambayo ni idara ya mazingira.
Alisema upo wasi wasi unaoonekana wazi wa bahari kuendelea kula eneo kubwa la ardhi kutokana na uchafuzi wa mazingira ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na tabia ya baadhi ya watu wasiozingatia utunzaji wa mazingira.
“ Huu ni utaratibu uliowekwa kisheria na Serikali. Hivyo lazima kwa uongozi wowote wa taasisi ya uwekezaji katika sekta ya Utalii ufuate taratibu ya Idaya ya Mazingira pamoja na Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } ili kuwepuka mapema matatizo kama hayo”. Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia tatizo la ardhi linalolalamikiwa na Wananchi wa Uroa dhidi ya Uongozi wa Hoteli hiyo ya Malumbo Reef Balozi Seif alisema Zanzibar hivi sasa imechoshwa na haihitaji tena kuendelea kuwa na migogoro ya ardhi.
Alisema Serikali imefikia uamuzi wa sehemu ya ardhi yake ndogo iliyonayo kutumiwa kwa ajili ya sekta ya Utalii ili kusaidia Uchumi wa Taifa ambao bado unategemea zao la Karafuu na migogoro iliyopo sasa lazima ifuatiliwe na kutafutiwa suluhisho la kudumu.
Balozi Seif alisisitiza kwamba mategemeo ya Taifa kwa ujumla ni kuona mapato yatokanayo na sekta ya Utalii yanaifaidisha Serikali sambamba na wananchi wote badala ya kuona neema hiyo inakwenda na kuingia mikononi kwa muekezaji pekee.
“Mapato ya Utalii lazima yaifaidishe Serikali ambayo ndio iliyoamua kutumia ardhi yake chache iliyokuwa nayo kwa kupanua sekta ya utalii kwa mategemeo ya kuongeza mapato kwa wadau wote wa sekta hiyo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Hoteli ya Palumbo Reef kwa juhudi zake za kuwa karibu na wananachi wa eneo hilo hali inayojenga mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya Utalii kati ya wageni na wenyeji husika.
Mapema Mkurugenzi wa Hoteli ya Palumbo Reef Bwana Shaaban Haji Kitwana alisema tatizo kubwa linalojitokeza ambalo hata halihitaji ufumbuzi wa ngazi za juu za Serikali ni kwa baadhi ya wazawa kuwa na tabia chafu ya kuwahadaa kimaarifa wenzao wakati wanapouza mali zao kwa ajili ya uwekezaji.
Bwana Shaaban alisema ipo mikataba wanayokubaliana na Wananachi hao inayofikia maamuzi sahihi lakini baadaye huchipuka mzozo kati ya wazawa hao na hjatimae kuwahusisha wawekezaji wasiostahiki kuwemo kwenye mzozo huo.
Naye kwa upande wake Mmiliki wa Hoteli hiyo Bwana Palumbo Sila alimueleza Balozi Seif kwamba mazingira na ukarimu uliopo Zanzibar ndio chachu inayowahamasisha wawekezaji wengi wa nje kuja kuwekeza vitega uchumi vyao hapa Nchini.
Bwana Mapumbo alisema katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na tatizo la ajira Uongozi wa Hoteli hiyo umeamuwa kuwapa kipaumbele Wananchi Wazalendo katika shughuli za uendeshaji wa Hoteli hiyo kwa zaidi ya asilimia 99.9%.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/1/2013.
No comments:
Post a Comment