Na
Zawadi Msalla-MAELEZO-Dar
Wanafunzi waliowahi kusoma katika
shule ya Sekondari Enaboishu ya jijini Arusha wanatarajia kukutana tarehe 5
Desemba 2015 ili kujadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuisaidia shule
hiyo katika kuboresha maendeleo ya taaluma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Muda wa Jumuiya hiyo ya Enaboishu Renalda Shirima
alisema mkutano huo wa kwanza utafanyika katika matawi mawili ya mkoa wa Arusha
na Dar es salaam.
Ambapo katika mkoa wa Dar es salaam
utafanyika katika ukumbi wa Triple Seven eneo la Kawe na Arusha katika club ya AICC Kijenge.
Renalda alisema jumuiya hiyo ina
malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuangalia fursa mbalimbali ambazo
wanaweza kushirikiana katika kuleta maendeleo ya taaluma katika shule yao ya
zamani kwa kuboresha mazingira ya wanafunzi na walimu ya kujifunzia na
kufundishia.
“Tutaweza kufahamiana kwa karibu zaidi
kwa watakao hudhuria na pia kupata mawasiliano ya wale ambao hawata hudhuria,
hii pekee ni chachu ya kuleta maendeleo” alisema Renalda.
Aliongeza kuwa kwa sasa zipo
changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ambazo kwa pamoja kama Taifa ni
lazima kuungana ili kuweza kuisaidia Serikali katika kuzitatua. Jumuiya hiyo ya
wana Enaboishu imedhamiria kwa dhati kulipa fadhila katika shule yao ili
kuondoa changamoto hizo.
Aidha alisema wanatajaria kuweka
mkakati wa kuishauri Serikali namna ya kuwatumia wahitimu wa zamani wa shule mbalimbali
nchini ili kuboresha miundombinu ya shule walizo soma.
“Tungependa utamaduni huu sasa
ujengeke na uenee nchi nzima” Alisema.
Mwenyekiti huyo wa muda alisema katika
kikao hicho pia wanatarajia kuchagua uongozi wa kudumu wa umoja huo.
Shule ya Sekondari ya Enaboishu
imeanzishwa mwaka 1966. Mpaka sasa shule hiyo imeshatoa wahitimu ambao wako
katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani na nje ya nchi. Baadhi ya viongozi
wakubwa walio wahi kusoma katika shule hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni
na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel.

No comments:
Post a Comment